Breaking

Monday, 28 April 2025

WAZIRI KIKWETE AIPONGEZA BARRICK KWA MATUMIZI TEKNOLOJIA ZENYE USALAMA MIGODINI

Mtaalamu wa Afya na Mazingira kutoka Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Aristides Medard (Kushoto) akifafanua jinsi mgodi huo wa Barrick unavyofanya shughuli za uchimbaji kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu , vifaa na mitambo ya kisasa na akili mnemba kwa Waziri wa Nchini Ofisi ya Waziri Mkuu (Ajira, Kazi na Watu wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete ambaye alikuwa Mgeni Rasmi wa Maonesho yanayoendelea na Afya na Usalama mahali pa kazi yanayoratibiwa na Wakala wa Afya na Usalama wa Mahali pa kazi (OSHA) katika viwanja vya Mandewa mjini Singida
Waziri wa Nchini Ofisi ya Waziri Mkuu (Ajira , Kazi na Watu wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete akipata maelezo moja ya kifaa cha kukaa kinavyofanya kazi kwenye migodi ya Barrick North Mara
Mrakibu Mwandamizi wa Usalama wa Mgodi wa North Mara, Bw. Meshack Issack (kushoto) akitoa maelezo na ufafanuzi kuhusu akili mnemba inavyotumika kwenye uchimbaji wa madini kwenye migodi ya Barrick kwa Waziri wa Nchini Ofisi ya Waziri Mkuu (Ajira , Kazi na Watu wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete kwenye maonesho ya usalama mahali pa kazi yanayoendelea kwenye viwanja vya Mandewa mjini Singida

***
Waziri wa Nchini Ofisi ya Waziri Mkuu (Ajira, Kazi na Watu wenye Ulemavu) , Mhe Ridhiwani Kikwete ameipongeza migodi ya Barrick yenye ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga nchini kwa kuboresha utendaji kazi wake kwa kutumia Akili Mnemba (AI) na vifaa, mitambo ya kisasa ya kijiditali na kulinda usalama na afya za wafanyakazi wake mahali pa kazi.

Amesema hayo alipotembelea banda la Barrick kwenye maonesho ya OSHA yanayoendelea kwenye viwanja Mandewa mjini Singida na kusisitiza umuhimu wa kuweka mfumo madhubuti wa teknolojia ili kulinda afya za wafanyakazi kwenye sehemu zote za kazi kama vile migodi, viwandani na sehemu zingine.

“Huko nyuma mlikuwa mnakwenda wenyewe chini kwenye uchimbaji wa dhahabu chini ya ardhi lakini sasa mnatumia mitambo ili kuweza kufanikisha kazi hii, hongereni sana kwa kuboresha mazingira ya kufanyia kazi,” amesema Kikwete alipokuwa kwenye Banda la Barrick Bulyanhulu.

Mhe. Kikwete aliongeza kwamba juhudi za Barrick nchini kwa kushirikiana na Wakala wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) zimefanikisha kuwepo mazingira rafiki ya ufanyaji kazi ambayo ni chachu katika kuleta mabadiliko Chanya katika sekta ya uchimbaji wa madini,

“Natoa wito kwamba elimu hii ya afya na usalama mahali pa kazi inayoendelea kutolewa kupitia maonesho haya iendelee kutolewa nchini nzima ili kupanua wigo wa uelewa kwa watanzania hasa wafanyakazi katika sekta mbalimbali hapa nchini katika kukabiliana na ajali na majanga sehemu za kazi,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Aristides Medard, Mtaalam wa Afya na Mazingira kutoka mgodi wa Barrick Bulyanhulu amemweleza Waziri Kikwete na ujumbe wake kuwa kwa kutumia akili mnemba mgodi huo unaendesha shughuli zake kwa ufanisi na usalama zaidi hali ambayo inawapa motisha wafanyakazi kufanya kazi kutokana na mazingira kuwa rafiki.

Naye Mrakibu Mwandamizi wa Usalama, Bw. Meshack Issack kutoka Mgodi wa North Mara amesema mgodi huo ni kinara wa matumizi ya kidigitali na akili mnemba na mifumo ya kimataifa katika uchimbaji wa madini na afya na usalama nchini.

Ameongeza kwamba mgodi huo na migodi mingine yote ya Barrick inatekeleza program ya “Journey to Zero” ambayo inalenga kuhakikisha kila mfanyakazi anakuwa salama kazini hadi anaporudi nyumbani na kupaza sauti kunapokuwepo na viashiria vya mazingira hatarishi kwenye maeneo ya kazi.

“Hii programu ya “Journey to Zero” ni DNA ya kampuni inawahusu pia wakandarasi wa Barrick ,wageni wanaotembelea migodi yetu na jamii nzima kwa ujumla”, amesisitiza.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages