Breaking

Tuesday, 8 April 2025

WAZIRI DKT. GWAJIMA AAMSHA ARI YA WANAWAKE KUJIUNGA MAJUKWAA YA UWEZESHAJI WANAWAKE KICHUMI

   

•Apokea nakala 1000 za Mwongozo wa Uundaji na Uanzishwaji wa Majukwaa ya Uwezeshaji wa Wanawake kiuchumi.

•Atambulisha Kamati ya Kitaifa ya kuratibu hamasa na elimu kwa Wanawake kujiunga na Majukwaa hayo.

Na WMJJWM- Dar es Salaam

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewataka Wanawake kujiunga na Majukwaa ya Uwezeshaji wa Wanawake kiuchumi Ili kuzifahamu fursa za kiuchumi zilipo nchini. 

Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo Aprili 08, 2025 jijini Dar Es Salaam wakati akipokea nakala 1000 za Mwongozo wa Uundaji na Uanzishwaji wa Majukwaa ya Uwezeshaji wa Wanawake kiuchumi kutoka Benki ya Biashara Tanzania (TCB) na kuitambulisha 
Kamati ya Kitaifa ya kuratibu Hamasa na Elimu kwa Wanawake kujiunga na Majukwaa hayo.
 
Waziri Dkt. Gwajima amesema, lengo la Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona Wananchi wanazifahamu fursa mbalimbali za kujikwamua kiuchumi likiwemo kundi la Wanawake.
Akizungumzia kwenye hafla hiyo, Waziri Dkt. Gwajima amesema, jukumu la Kamati hiyo ya kitaifa ni kuratibu Wadau wengine wote kushiriki kwenye zoezi hili endelevu la kuhamasisha na kutoa elimu kwa wanawake walio kwenye majukwaa ya uwezeshaji kiuchumi ili wafahamu faida za kujiunga kupitia Kampeni ya ‘Inuka-Imarika-Tusua Kiuchumi’.

“Natoa wito kwa  Wadau wote wa maendeleo kushirikiana na Kamati hii niliyoitambulisha rasmi leo Aprili 8, 2025 ili iweze kufanya kazi yake kwa ufanisi mkubwa” amesema Dkt. Gwajima.

Ameongeza kwamba, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa maendeleo imekuwa ikitekeleza jukumu la kuwawezesha Wanawake Kiuchumi ambapo, kutokana na uzoefu wa utekelezaji huo ilifanya mapitio ya Mwongozo wa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi wa mwaka, 2022 na kutoa toleo la mwaka 2024 linaloendana na mahitaji ya sasa. 

Aidha Waziri Dkt. Gwajima ameishukuru Benki ya Biashara Tanzania kwa utayari wa kuchapisha nakala elfu moja (1000) za Mwongozo huo ambao usambazaji wake utaanza  rasmi  sambamba na kampeni ya hamasa na elimu na kufika ngazi zote hadi kata, vijiji na mitaa. 

"Nakala hizi zitasaidia ni nyezo muhimu katika uhamasihaji wa wanawake kujiunga katika majukwaa ya uwezeshaji kiuchumi" amesema Waziri Dkt. Gwajima

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia Badru Abdulnoor amesema, Wizara itaendelea kushirikiana na Wadau katika kuhakikisha Sera na Mipango ya Serikali kuhusu uwezeshaji Wanawake kiuchumi inatekelezwa. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB) Adam Mihayo amesema, Benki hiyo imefanya maboresho katika afua zake za kuhakikisha inaendeleza juhudi  za Serikali katika kuwawezesha Wanawake kiuchumi na kwa mwaka 2024 Benki hiyo ilitoa shillingi bilioni 300 kuwawezesha Wanawake kiuchumi.

Benki ya Biashara Tanzania (TCB) imedhamini uchapishaji wa Mwongozo wa Majukwa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi nakala 1,000 ili kuweza kutoa Elimu juu ya utekelezaji wa majukumu hayo nchini.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages