Breaking

Friday, 11 April 2025

UMOJA WA ULAYA NA TANZANIA KUSHAMIRISHA USHIRIKIANO KUBORESHA MIJI JUMUISHI, KIJANI NA JANJA NCHINI TANZANIA

Ujumbe wa ngazi ya juu wa Wakuu wa Ushirikiano kutoka Umoja wa Ulaya umetembelea miradi ambayo umoja huo unafadhili katika jiji la Mwanza ili kuimarisha ushirikiano wa EU na Tanzania wenye lengo la kuendeleza uwekezaji katika maendeleo endelevu ya miji.

Katika ziara hiyo ujumbe huo na mwenyeji wao, uongozi wa mkoa wa Mwanza umtembelea mtambo wa kutibu maji uliopo Butimba na kuzindua Ofisi ya Programu ya  Miji jumuishi na kijani (Green and Smart Cities-SASA) jijini Mwanza.

Mtambo wa  Kutibu Maji wa Butimba   ni uwekezaji mkubwa chini ya Mradi wa wa Mazingira wa Ziwa Victoria, unasambaza maji safi ya bomba kwa karibu watu 500,000 kwenye vitongoji wa kusini vya jiji la Mwanza.

Katika ziara ya TeamEurope pia ofisi ya Program ya Miji Kijani na Janja (SASA) ya jijini Mwanza ilizinduliwa. Ofisi hiyo ya pamoja itaimarisha uratibu na ushirikiano kati ya washirika wa utekelezaji wa miradi ya program ya SASA jijini Mwanza. 

Mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, aliwakilishwa na Afisa Tawala Msaidizi wa Mkoa, anayeshughulikia Viwanda, Uwekezaji na Biashara, Bw. Martin Karangwa.

 Hafla ya uzinduzi wa ofisi hiyo iliwakutanisha wakuu wa ushirikiano kutoka Ubelgiji, Denmark, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Sweden na Uholanzi.

Bw. Karangwa alisema, Uongozi wa Mkoa wa Mwanza utahakikisha kwamba ushirikiano unaendelezwa na kuhakikisha rasilimali na utaalamu katika program ya SASA vinaleta matokeo yanayotarajiwa.

"Nina matumaini makubwa kwamba matokeo ya SASA yatakuwa endelevu na  ya kuigwa na miji mingine nchini Tanzania, kwa sababu programu hii na miradi yake inaboresha ujuzi kutokana na mahitaji halisi ya Tanzania," alisema.

Mbali na mradi wa maji na usafi wa mazingira, SASA imesaidia uboreshaji wa soko la samaki la Mwaloni na machinjio ya Jiji la Mwanza.

"Kupitia mpango wa SASA, tunasaidia miji kuwa jumuishi zaidi, thabiti, na kuwa na kujiandaa kukidhi mahitaji ya ongezeko la watu," alisema Marc Stalmans, Mkuu wa Ushirikiano wa EU. 

Marc Stalmans, Mkuu wa Ushirikiano wa EU

"Ushirikiano huu sio tu kuhusu miundombinu-ni kuhusu utu, upatikanaji wa huduma, na fursa kwa watu wa Tanzania.", alisema.

Mwanza ni moja kati ya majiji yanayokua kwa kasi Kusini mwa Jangwa la Sahara, Afrika. Benki ya Dunia inakadiria kuwa idadi ya watu itaongezeka maradufu ifikapo 2035.

"Mwanza inahitaji mipango miji inayostahimili athari za mabadiliko ya tabia nchi ili kutoa huduma muhimu kwa wananchi wake. 

Mifumo ya usambazaji wa maji inabidi idhibiti upotevu wa maji, na huduma ya usafi wa mazingira inapaswa kuwafikia wateja wake," alisema Tobias Godau, Meneja Programu wa GIZ wa Maji na Mabadiliko ya Tabianchi. Alimwakilisha Mkurugenzi wa GIZ Tanzania katika hafla hiyo.

Mkurugenzi wa Enabel nchini Tanzania, Koenraad Goekint alisema, "Mpango huu unawakilisha hatua muhimu katika juhudi zetu za pamoja za kukuza maendeleo endelevu ya mijini. 

Mradi wa Miji ya Kijani na Jumuishii sio tu kuhusu kuboresha miundombinu ya kisasa; ni kuhusu kuunda maeneo ya mijini yanayostahimili, jumuishi, na rafiki kwa mazingira ambayo yanaweza kustawi na kukabili changamoto za siku zijazo."

Mkurugenzi wa Enabel nchini Tanzania, Koenraad Goekint

Mpango wa Green and Smart Cities SASA umeundwa ili kuboresha maisha ya mijini Mwanza, Tanga, na Pemba, kuunga mkono juhudi za Tanzania kukabiliana na ukuaji wa haraka wa miji. 

Mpango huo wenye thamani ya zaidi ya TZS 813 bilioni (EUR 325 milioni) unalenga katika kupanua utoaji wa huduma mijini, kuongeza mapato ya ndani na fursa za kiuchumi kwa wanawake na vijana. 

Jijini Mwanza, lengo la SASA ni kujenga uchumi endelevu wa ndani—kuimarisha usindikaji wa chakula, kusaidia sekta ya uvuvi, na kukuza uchumi wa mzunguko. 

Mipango hii imeundwa ili kuzalisha ajira, kukuza biashara za ndani, na kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi unajumuisha wengi na ni rafiki kwa mazingira.

Timu ya Ulaya (#TEAMEUROPE) ni mkakati  shirikishi inajumuisha  taasisi ya Umoja wa Ulaya, Nchi Wanachama wake, na mashirika ya maendeleo ili kutoa ushirikiano wa maendeleo ulioratibiwa kwa pamoja.

Kutumia ofisi ya pamoja iliyozinduliwa leo kutawezesha ushirikiano kati ya mashirika yanayotekeleza Mpango wa SASA, ambayo ni GIZ kutoka Ujerumani, Enabel kutoka Ubelgiji na AFD kutoka Ufaransa.

Afisa Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mwanza, anayeshughulikia Viwanda, Uwekezaji na Biashara, Bw. Martin Karangwa akizungumza
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages