NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
ASASI za Kiraia, Mashirika pamoja na wadau wanaojihusisha na utetezi wa wanawake wamesisitiza uhitaji wa serikali kuzingatia ujumuishaji na utekelezaji wa masuala ya kijinsia kwa vitendo katika bajeti ya kitaifa na kuhakikisha zinagusa wananchi.
Hayo yamebainishwa leo Aprili 11, 2025 Jijini Dar es Salaam kwenye kikao cha kujadili bajeti ya mwaka 2025/26 inayojali usawa wa kijinsia, ikiwa ni sehemu ya tathmini ya mafanikio ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 (TDV 2025) na maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 (TDV 2050) kilichoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).
Kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali kutoka asasi za kiraia, wataalamu wa sera, na wawakilishi wa makundi ya wanawake, kikilenga kuchambua namna bajeti imekuwa chombo cha mabadiliko ya kijamii, hasa kwa wanawake. Taarifa zilitolewa kuonyesha kuwa ushiriki wa wanawake kwenye kazi za kipato umeongezeka kutoka asilimia 67 mwaka 2000 hadi asilimia 80.2 mwaka 2023 – mafanikio yanayoashiria nguvu ya bajeti jumuishi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Bi. Gema Akilimali alisema: “Bajeti yenye mtazamo wa kijinsia huanzia kwenye upangaji hadi utekelezaji wake. Ni muhimu wanawake na makundi maalum kushirikishwa kikamilifu katika hatua zote za mchakato huo.”
Aliongeza kuwa changamoto kubwa inabaki kuwa utoaji wa fedha halisi ikilinganishwa na makadirio. “Makadirio huwa makubwa, lakini fedha zinazotolewa ni ndogo. Kazi yetu ni kuhakikisha tunafuatilia matumizi ya fedha hizo ili kuhakikisha zinatumikia lengo lililokusudiwa,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Bi. Lilian Liundi, alisisitiza kuwa ili Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 iwe jumuishi, ni lazima misingi ya usawa wa kijinsia izingatiwe kuanzia sasa. “Tunapojadili bajeti na dira mpya, tunapaswa kujiuliza: Je, wanawake wana nafasi gani katika michakato ya maamuzi? Je, rasilimali zinaelekezwa kwa kuzingatia mahitaji ya wote?” alihoji.
Alisema TGNP itaendelea kushirikiana na serikali na wadau kuhakikisha sauti za wanawake zinahesabiwa.
“Tunataka kuona wanawake wakiwa mstari wa mbele sio tu kama walengwa, bali kama wachangiaji wakuu wa maendeleo ya nchi,” aliongeza Liundi.
Mijadala ya kina pia iligusia mafanikio mengine kama vile kuongezeka kwa wanawake wanaojihusisha na taaluma za kihandisi, na uboreshwaji wa mifumo ya mikopo kupitia sheria za fedha za serikali za mitaa.
Hata hivyo, changamoto zimeendelea kujitokeza – hususan urasimu katika upatikanaji wa mikopo ya 4-4-2, umiliki duni wa ardhi kwa wanawake (asilimia 8 pekee), na ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu bajeti za jinsia.
Katika bajeti ya mwaka 2025/26 yenye thamani ya Sh trilioni 57.02, Serikali imeweka vipaumbele vya kukuza usawa wa kijinsia na kuwezesha makundi maalum.
Hata hivyo, TGNP imesisitiza kuwa kuna mapungufu katika kugharamia sekta muhimu kama viwanda, biashara na hifadhi ya jamii – maeneo ambayo ni nguzo za uchumi shindani na jumuishi.
Katika karatasi ya majadiliano iliyoandaliwa na mtaalamu wa sera za kijinsia, Makumba Mwemezi, inabainika kuwa licha ya hatua zilizopigwa kwenye sekta ya elimu, changamoto bado ni kubwa.
“Zaidi ya wanafunzi 148,000 waliripotiwa kuacha shule mwaka 2023 licha ya sera ya elimu bila malipo,” alisema, akisisitiza umuhimu wa ubora na ujumuishi katika elimu.
Kwa upande wa maji, alisema: “Upatikanaji wa maji safi vijijini umeongezeka kutoka asilimia 53 mwaka 2003 hadi asilimia 72 mwaka 2022. Hata hivyo, theluthi moja ya vyanzo vya maji havifanyi kazi ipasavyo.”
Mwemezi alipendekeza Tanzania iwe na Mpango Maalum wa Kitaifa wa Usawa wa Kijinsia (GEWE) badala ya kuacha masuala ya jinsia kuwa sehemu ya vipengele ndani ya sekta mbalimbali. “Hili ni muhimu kwa maendeleo endelevu,” alisisitiza.
Mapendekezo kutoka Wajibu Institute, kama yalivyowasilishwa na Karoli Kadenge, yanaitaka serikali kuhakikisha mgao na matumizi sahihi ya rasilimali zilizopo katika kipindi kilichosalia cha FYDP III. Kadenge alisema: “Serikali inapaswa kutathmini upya vipaumbele vya maendeleo na kuelekeza zaidi fedha katika huduma za kijamii kama afya, elimu na maji.”
Kikao hicho kimehitimishwa kwa wito wa kuhakikisha kwamba katika safari ya kuelekea TDV 2050, wanawake hawaachwi nyuma, bali wanakuwa sehemu ya mabadiliko ya kiuchumi na kijamii kwa usawa kamili.