Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imepongezwa kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo ya elimu kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa pamoja na Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF).
Pongezi hizo zimetolewa leo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Methusela Ntonda, alipotembelea banda la TEA katika ufunguzi wa Maonesho ya Kitaifa ya Kazi za Utamaduni na Sanaa yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Jijini Dar es Salaam.
Akiwa kwenye banda hilo, Ntonda alipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na TEA, zikiwemo taarifa za miradi ya elimu na Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi, pamoja na bidhaa zilizotengenezwa na mmoja wa wanufaika aliyepata ufadhili wa kusomea Mafunzo ya Kuendeleza Ujuzi.
Aidha, Ntonda amesema amevutiwa na juhudi za Mamlaka hiyo katika kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia, sambamba na uwezeshaji uliotolewa kwa Watanzania kupitia ufadhili wa mafunzo ya ujuzi.
Bw. Ntonda aliipongeza TEA na kusema uwekezaji uliofanywa kupitia mifuko yote miwili una mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya sekta ya elimu na kukuza maarifa kwa wananchi, hasa vijana. Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza jitihada hizo kwa kushirikisha wadau mbalimbali ili kuhakikisha elimu bora na fursa za ujuzi zinapatikana kwa watu wengi zaidi nchini.
Awali, akitoa utambulisho wa Mamlaka hiyo, Afisa Uhusiano na Mawasiliano wa TEA, Bi. Eliafile Solla alisema, TEA ilianzishwa kwa lengo la kusimamia Mfuko wa Elimu wa Taifa, ambapo majukumu yake makuu ni kutafuta rasilimali fedha kutoka kwa wadau wa ndani na nje ya nchi, pamoja na kuzitumia kusaidia juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu nchini. Aliongeza kuwa TEA pia ina jukumu la kuratibu na kusimamia utekelezaji wa miradi ya uendelezaji ujuzi kupitia Mfuko wa SDF.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Methusela Ntonda akisikiliza Maelezo kutoka kwa Bi. Eliafile Solla alipotembelea banda la Mamlaka ya Elimu Tanzania kwenye ufunguzi wa maonesho ya Kazi za Utamaduni na Sanaa.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Methusela Ntonda akiangalia moja ya bidhaa ya mnufaika wa SDF alipotembelea banda la Mamlaka ya Elimu Tanzania kwenye ufunguzi wa maonesho ya Kazi za Utamaduni na Sanaa.
Bi Ester Shebe Mnufaika wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi uliokuwa ukiratibiwa na TEA akitoa maelezo ya bidhaa zake kwa Mgeni Rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Methusela Ntonda.
Afisa Uhusiano na Mawasiliano Bi. Eliafile Solla akitoa zawadi kwa Mgeni Rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Methusela Ntonda alipotembelea banda la Mamlaka ya Elimu Tanzania kwenye ufunguzi wa maonesho ya Kazi za Utamaduni na Sanaa.