NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi TBS, Prof. Othman Chande amewataka wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini kuendelea kushiriki katika mashindano ya uandishi wa insha kuhusu viwango ambayo yanafanyika kila mwaka ili kuongeza uelewa juu ya viwango na mchango wake katika kulinda afya ya jamii, usalama na kuwezesha biashara.
Ameyasema hayo leo Aprili 4, 2025 Jijini Dar es Salaam wakati wa Kilele Cha Maadhimisho ya Siku ya Viwango Afrika ambayo imejumuisha zoezi la kutoa zawadi kwa washindi wa shindano la insha.
"Ninachukua fursa hii kuwapongeza wanachuo wote walioshiriki katika shindano hili. Ninawapongeza zaidi washindi ambao insha zao zimechaguliwa kwenye kundi la washindi kumi bora". Amesema Prof. Chande.
Aidha Prof. Chande ametoa wito kwa TBS kuendelea kuhusisha wadau kwa kuzingatia nyanja zote husika katika utaratibu wa uandaaji wa viwango kwani viwango vina mchango mkubwa katika fursa za uchumi ikiwa ni pamoja na kukabiliana na changamoto mbalimbali za maendeleo endelevu.
Amesema kuwa elimu ya viwango ni muhimu katika kutumia fursa mbalimbali za maendeleo ya taifa letu, pia huwezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali katika kukuza uchumi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS Dkt. Candida Shirima amezipongeza taasisi za elimu ya juu ambazo zimekuwa zikiwawezesha wanafunzi wake kushiriki katika shindano la uandishi wa insha tangu lilipoanzishwa.
Amesema wanafunzi wengi kutoka vyuo mbalimbali walishiriki na idadi yao imekuwa ikiongezeka kila mwaka hivyo inaashirika kuongezeka kwa mwamko na uelewa kuhusu masuala ya viwango.