Breaking

Friday, 11 April 2025

NELSON MANDELA YALETA TEKNOLOJIA YA UFUGAJI FANISI



Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na ya Teknolojia ya Nelson Mandela,Prof. Maulilio Kipanyula, akizindua rasmi Kituo cha Teknolojia ya kisasa ya ufugaji Fanisi kwa kumuingiza ng'ombe katika banda Aprili 11,2025 Kampasi ya Tengeru jijini Arusha.

........

TAASISI ya Afrika ya Sayansi na ya Teknolojia ya Nelson Mandela imezindua kituo maalum cha utafiti wa teknolojia za kisasa kwa ufugaji fanisi kinacholenga kutatua changamoto za ufuguji wa ng’ombe wa maziwa ikiwemo kutoa taarifa ya maradhi, chakula na muda sahihi wa joto kwa ajili kupandikiza.

Akizungumza wakati wa kuzindua kituo hicho Aprili 11, 2025 katika kampasi ya Tengeru, jijini Arusha, Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na ya Teknolojia ya Nelson Mandela,Prof. Maulilio Kipanyula, ameeleza kuwa, kazi kubwa ya taasisi hiyo ni kuzalisha teknolojia mpya pamoja na kuhuisha zilizopo lengo likiwa ni kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii pamoja na viwanda.

“Kituo hiki kitawezesha wafugaji wa ng’ombe wa maziwa kujifunza kwa kina namna ya kutumia teknolojia ya kisasa kupitia kifaa maalum cha donge kitakachowekwa kwenye tumbo la ng'ombe ili kujua kiasi sahihi cha chakula, maji na muda sahihi kupanda kwa joto kwa ajili ya upandikizaji" Prof. Kipanyula.

Aidha Prof. Kipanyula ameleza kuwa, kifaa hicho baada ya kuwekwa kwa mnyama hufungwa katika banda na kuunganisha mawasiliano katika simu hivyo kumuwezesha mfugaji kutembea na mifugo yake kiganjani kwa kupata taarifa muhimu zinazosaidia kujua na kutekeleza uhitaji kwa wakati.

"Teknolojia hii itasaidia kuondokana na changamoto ya kukisia kuhusu ulaji, unywaji na upandishaji joto kwa ng'ombe, jambo ambalo litaongeza uzalishaji wa maziwa pamoja na ndama" Anasema Prof. Kipanyula

Kwa Takwimu ng'ombe anatakiwa kupata ndama kila mwaka lakini kutokana na changamoto ya ulishaji na kupata taarifa kwa wakati kuhusu kupandishwa kwa joto la mnyama, wafugaji wamekuwa wakipata ndama kila baada ya miaka miwili hadi mitatu jambo ambalo linadunisha uzalishaji.

Naye Mratibu wa Mradi Prof. Gabriel Shirima ,ameeleza kuwa, mbali na kituo hicho mradi unawasimamia wafugaji 100 katika vijiji vitano vya Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro kwa kuwawezesha kifaa hicho maalum ili kupata taarifa sahihi kuhusu mnyama katika masuala ya lishe na joto.

“Kituo kitajikita katika kufanya utafiti, kutambua aina ya mifugo na ulishaji wake, kutambua ng’ombe akiwa ameingia joto kwa wakati , unywaji wa maji kwa mnyama, kuendeleza , kupima na kuhuisha teknolojia zilizopo pamoja na kutoa mafunzo kwa wafugaji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali “ amesisitiza Prof. Shirima

Kituo hiki cha tenknolojia kinafanya kazi chini ya Mradi wa tathmini ya ufanisi wa teknolojia za kisasa za ufugaji wa mifugo barani Afrika kwa ufadhili wa Bill na Melinda Gates Foundation nchini Marekani.



Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na ya Teknolojia ya Nelson Mandela,Prof. Maulilio Kipanyula, akizindua rasmi Kituo cha Teknolojia ya kisasa ya ufugaji Fanisi kwa kumuingiza ng'ombe katika banda Aprili 11,2025 Kampasi ya Tengeru jijini Arusha.



Naibu Makamu Mkuu wa Taasisi Taaluma, Utafiti na Ubunifu Prof. Anthony Mshandete,akiweka kifaa cha donge kwa ng'ombe ambacho kinasaidia kupata taarifa muhimu kuhusu uhitaji wa chakula, maji na upandaji wa joto wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Teknolojia ya Kisasa kwa Ufugaji Fanisi Aprili 11,2025 jijini Arusha.



Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na ya Teknolojia ya Nelson Mandela,Prof. Maulilio Kipanyula, akiongea na Waandishi wa habari wakati wa uzinduzi rasmi wa Kituo cha Teknolojia ya kisasa ya Ufugaji Fanisi Aprili 11,2025 Kampasi ya Tengeru jijini Arusha.



Mratibu wa Mradi wa tathmini ya ufanisi wa teknolojia za kisasa za ufugaji wa mifugo barani Afrika,Prof. Gabriel Shirima ,akitoa historia ya mradi wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Teknolojia ya kisasa ya Ufugaji Fanisi Aprili 11,2025 jijini Arusha.



Ng'ombe waliowekewa kifaa maalum cha ndonge chenye kuwezesha kupata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu ulishaji, maji na joto kupanda kwa mnyama wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Teknolojia ya Kisasa ya Ufugaji Fanisi Aprili 11,2025 Kampasi ya Tengeru jijini Arusha.

Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na ya Teknolojia ya Nelson Mandela,Prof. Maulilio Kipanyula ( katikati) akiwa katika picha ya pamoja na waratibu wa Mradi wa tathmini ya ufanisi wa teknolojia za kisasa za ufugaji wa mifugo barani Afrika kwa ufadhili wa Bill na Melinda Gates Foundation Aprili 11,2025 jijini Arusha mara baada ya uzinduzi wa Kituo.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages