Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bi. Zuhura Yunus leo ametembelea banda la kampuni ya GASCO ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika maonesho ya Wiki ya Usalama Mahala pa Kazi yanayoendelea Mkoani Singida.
Katika ziara hiyo, Bi. Zuhura Yunus alipata fursa ya kujionea jitihada mbalimbali zinazofanywa na GASCO katika kuhakikisha mazingira salama na yenye afya kwa wafanyakazi wake, sambamba na kuzingatia viwango vya usalama katika shughuli za uendeshaji na matenegezo ya mitambo ya UchakaXAtaji, Usafirishaji na Usambazaji Gesi Asilia hapa nchini
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu aliipongeza GASCO kwa kuonesha dhamira na juhudi madhubuti katika kulinda afya na usalama wa wafanyakazi wake, na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi hizo ili kulinda rasilimali watu na kuimarisha tija mahala pa kazi.
"Naipongeza GASCO kwa kujidhihirisha kama taasisi yenye dhamira ya kweli na juhudi za hali ya juu katika kulinda afya na usalama wa wafanyakazi wake. Hatua hizi si tu zinajenga mazingira bora ya kazi bali pia zinaakisi uelewa wa kina kuhusu umuhimu wa rasilimali watu katika maendeleo endelevu ya taasisi. Ni rai yangu kwamba juhudi hizi ziendelezwe na kuimarishwa zaidi, ili kuendelea kuhamasisha ustawi wa wafanyakazi na kuleta tija inayokusudiwa katika maeneo ya kazi." Alizema Yunus
Maonesho haya yamelenga kuhamasisha taasisi na mashirika yote nchini kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango vya usalama na afya kazini kwa ustawi wa wafanyakazi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Afisa Usalama na Mazingira Mahala Pa Kazi wa GASCO Bi: Zuzana Masaba akifafanua jambo kwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bi. Zuhura
Watumishi wa GASCO katika picha na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bi. Zuhura