Breaking

Friday, 11 April 2025

DKT. GWAJIMA AITAKA JAMII KUZITUMIA HUDUMA ZA USTAWI WA JAMII KUTATUA CHANGAMOTO ZA KIFAMILIA

      


Na WMJJWM-Mtwara

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, ameitaka jamii kutambua na kutumia kikamilifu huduma zinazotolewa na wataalamu wa Ustawi wa Jamii ili kutatua changamoto mbalimbali, hususan migogoro ya kifamilia inayochangia ongezeko la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.

Dkt. Gwajima ametoa wito huo leo, Aprili 11 2025, wakati wa ufunguzi wa mdahalo wa kijamii Mkoani Mtwara kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto Anayeishi na Kufanya Kazi Mtaani, ambayo yamepangwa kufanyika  Aprili 12 mkoani humo.

Amesema kuwa jukumu la kulinda na kuhakikisha usalama wa mtoto ni la jamii nzima, na kwamba Sheria ya Mtoto Sura ya 13 inatamka wazi wajibu wa mzazi katika malezi ya mtoto. 

Aidha, amebainisha kuwa mzazi au mlezi anayeshindwa kutekeleza majukumu hayo hukabiliwa na adhabu ya faini isiyozidi Shilingi Milioni 5, kifungo cha hadi miezi 6, au adhabu zote kwa pamoja.
"Mdahalo huu unatoa elimu sahihi kwa wazazi na walezi kuhusu malezi bora ya watoto, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhamasisha malezi chanya. Tunataka jamii ibadili mtazamo wake na kuunda mazingira salama yanayomlinda mtoto dhidi ya kuingia mitaani, kupata mimba za utotoni au kukatisha masomo" amesema Dkt. Gwajima.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala, amesema mkoa huo umeweka mikakati endelevu ya kukabiliana na changamoto ya watoto wa mitaani, ikiwemo kutoa elimu kwa wazazi na walezi kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii ili kuimarisha malezi bora na kulinda haki za watoto kwa mujibu wa sheria.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, amesema mdahalo huo umeonesha kuwa na tija kubwa kwa ustawi wa watoto, na kwamba maoni yote yaliyotolewa na wadau yatapitiwa na timu ya wataalamu kwa lengo la kuyafanyia kazi na kuandaa mikakati ya kudumu ya kutokomeza tatizo hilo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages