Breaking

Wednesday, 16 April 2025

AfCFTA KUKAMILISHA KANUNI ZA UASILI WA BIDHAA ZA NGUO NA MAVAZI 



Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Seleman Jafo,akizungumza wakati akihutibia Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la AfCFTA uliofanyika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC) jijini Kinshasa

.......

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Seleman Jafo (Mb.) ametoa rai kwa Wataalamu wa Eneo huru la Biashara Afrika (AfCFTA)kuhakikisha majadiliano kuhusu Kanuni za Uasili wa Bidhaa za Nguo na Mavazi yanakamilika ili kutoa fursa kwa wafanyabiashara na wazalishaji wa nguo na mavazi kuzalisha kwa wingi na kupunguza uagizaji wa nguo na mavazi ikiwemo nguo zilizotumika.

Aidha amesisitiza kuendelea kuzihamasisha nchi sita (6) Barani Afrika zilizosalia kukamilisha mchakato na kuridhia mkataba huo ulioridhiwa na Nchi 48 ili kuharakisha utekelezaji wa Mkataba huo na kuchochea maendeleo ya uwekezaji, viwanda, biashara na kuimarisha uchumi ndani ya Afrika.

Waziri Jafo ameyasema hayo wakati akihutubia katika Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la AfCFTA lililofanyika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC) jijini Kinshasa ambapo Tanzania imekuwa mwenyekiti kwa mwaka 2024 na kukabidhi Uenyekiti huo kwa Misri 2025

Aidha katika kipindi hicho cha Uenyekiti, Waziri Jafo amebainisha kuwa AfCFTA imefanikiwa kukamilisha Kiambatisho cha Itifaki ya Uwekezaji cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji, Itifaki ya Biashara Mtandao, Kuridhia Kanuni za Mawaziri za kutoa upendeleo maalum wa soko kwa wafanyabiashara Wanawake na Vijana, Kuanzisha utaratibu wa mapitio ya utekelezaji wa Mkataba huo na Chombo cha Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara.

Mpango wa kuhamasisha biashara ndani ya AfCFTA (GTI) unaotumiwa na Nchi Wanachama 39 umefanikiwa katika kuwawezesha wafanyabiashara kuchangamkia fursa zilizopo na kuongezeka kwa bidhaa kutoka kilimo hadi za viwandani kama vile kemikali, vifaa vya kieletroniki, betri na vigae. amesema Dkt Jafo.

Kwa Tanzania hadi Januari 2025 imefanikiwa kuwa na Jumla ya Makampuni 43 ambayo imeweza kuuza bidhaa zake katika nchi mbalimbali za Afrika kupitia Mkataba huo kwa kutumia cheti cha uasili wa bidhaa cha AfCFTA ambapo, jumla ya vyeti 226 vimeweza kutolewa kwa Kampuni hizo. Bidhaa ambazo zimeuzwa kwa wingi kupitia vyeti hivyo ni nyuzi za katani tani 6,150 kwenda nchi za Nigeria, Ghana, Morocco na Misri; Vioo (Float Glasses) tani 1,433 kwenda Misri; Mchele tani 433 kwenda Burkina Faso na Cote d’ivoire; na kahawa tani 273.3 kwenda nchini Algeria.

Mafanikio haya yamewezekana kutokana na juhudi za Serikali yetu inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wafanyabiashara wetu na sera za kimkakati zilizowekwa na serikali kwa kushirikiana na Sekretarieti ya AfCFTA.

Aidha, amebainisha kuwa AfCFTA imefanikiwa kuanzisha utaratibu wa kuwepo na Kampuni za Biashara (AfCFTA Trading Companies -ATC) ambao umesaidia kuanzisha makampuni ya biashara katika nchi za Kenya, Ghana, Misri na Rwanda na iko mbioni kukamilisha majadiliano ya ufunguaji wa Soko la Biashara ya bidhaa.



Rais wa Jamhuri ya Kongo (DRC) Mhe. Felix Antonio Tshisekedi akisalimiana na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo(Mb) Aprili 15, 2025 mara alipowasili kwa ajili ya kufungua rasmi Mkutano wa 26 wa Eneo huru la Biashara Afrika wa Baraza la Mawaziri wa Biashara wa AfCFTA uliofanyika, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Kinshasa



Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Seleman Jafo,akizungumza wakati akihutibia Mkutano wa 16 wa Baraza la Mawaziri la AfCFTA uliofanyika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC) jijini Kinshasa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages