
Na, Mwandishi Wetu - SINGIDA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amewasihi vijana wanufaika wa mafunzo ya ufundi stadi kuzingatia ujuzi wanaopatiwa vyuoni ili waweze kuweza kujiajiri ama kuanzisha shughuli ambazo zitawaingizia kipato.
Aidha, amewataka vijana hao kuhakikisha wanafanya vizuri katika mafunzo hayo yanatolewa kwa muda wa miezi sita katika fani mbalimbali.
Mhe. Kikwete ametoa wito huo Machi 23, 2025 alipotembelea chuo cha ufundi stadi na marekebisho cha Sabasaba mkoani Singida kwa lengo la kukagua maendeleo ya wananufaika na programu ya Taifa ya kukuza ujuzi inayotekelezwa na Ofisi hiyo.
Waziri Ridhiwani Kikwete amesema, dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuwawezesha nguvu kazi ya taifa hususan vijana kiujuzi, hivyo katika mwaka wa fedha 2024/25 imetoa shilingi bilioni 9 kwa ajili ya kugharamia mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa kupitia programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi ambayo ili kuwezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
“Nimefurahi kuona vijana wamekuwa na mwitikio chanya na wamejitokeza kwa wingi sana kupata ujuzi na tumeshuhudia kwenye baadhi ya fani zimekuwa zikihusisha vijana wa kike, kiume na pia wenye mahitaji maalumu,”
Akiwasilisha taarifa ya chuo, Mkuu wa Chuo, Fatuma Malenga, amesema chuo hiko kimepanga kuwaunganisha vijana hao na halmashauri ili watakapohitimu waweze kunufaika na fursa zilizopo katika mkoa huo.
Naye kijana mnufaika, Yusuf Mohammed ameshukuru serikali kuwawezesha mafunzo hayo na pia ameomba muda wa programu hiyo uongezwe ili vijana wengi zaidi wanufaike na programu hiyo.
Katika ziara hiyo, Mhe. Ridhiwani Kikwete ametembelea pia chuo RC Mission VTC Manyoni kukagua maendeleo ya mafunzo hayo yanayotolewa kwa vijana.










