WATUMISHI wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) wamehimizwa kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano ili kufanikisha malengo yaliyowekwa katika mpango kazi wa taasisi hiyo.
Ushauri huu umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dkt. Erasmus Kipesha, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, wakati wa kikao cha nne cha baraza hilo kilichofanyika leo, Machi 10, 2025, mkoani Morogoro.
Akizungumza na wajumbe wa baraza hilo, Dkt. Kipesha alisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya idara na vitengo mbalimbali ndani ya mamlaka kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji.
Alibainisha kuwa majukumu mengi ya TEA ni mtambuka, yanayohitaji ushirikiano wa karibu kati ya idara moja na nyingine, hivyo ni muhimu kwa kila mtumishi kuwa tayari kutekeleza majukumu yoyote yatakayoelekezwa kwake.
Katika kikao hicho, wajumbe walipitia na kujadili taarifa mbalimbali za utekelezaji kutoka katika idara na vitengo vya mamlaka na kutoa maoni yao. Lengo kuu lilikuwa ni kutathmini hali halisi ya utekelezaji wa majukumu ya mamlaka na kubaini changamoto pamoja na fursa zilizopo katika kufikia malengo yake.
Aidha, wajumbe walijadili mbinu bora za kuboresha utendaji kazi wa TEA ili kuongeza tija katika sekta ya elimu. Majadiliano yalihusisha hatua zilizochukuliwa na mafanikio yaliyopatikana, pamoja na mikakati ya kuimarisha mchango wa TEA katika kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia nchini.
Kwa kuzingatia umuhimu wa ushirikiano na uwajibikaji, Dkt. Kipesha aliwahimiza watumishi wote wa TEA kuendelea kujituma na kushirikiana ili kuhakikisha malengo ya mamlaka yanafikiwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya elimu nchini.
Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Dkt. Erasmus Kipesha akisisitiza jambo wakati wa kikao cha baraza hilo kilichofanyika mkoani Morogoro
Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Dkt. Erasmus Kipesha akisisitiza jambo wakati wa kikao cha baraza hilo kilichofanyika mkoani Morogoro
Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa TEA wakifuatilia uwasilishaji wa taarifa mbalimbali kwenye kikao kilichofanyika mkoani Morogoro
Kaimu Mkurugenzi Huduma za Taasisi CPA. Mwanahamis Chambega (kulia) akitoa ufafanuzi wa jambo kwa Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wakati wa kikao kilichofanyika mkoani Morogoro. Kushoto ni Mkaguzi Mkuu wa ndani CPA. Richard Mazinge
Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa TEA wakifuatilia uwasilishaji wa taarifa mbalimbali kwenye kikao kilichofanyika mkoani Morogoro