Breaking

Monday, 3 March 2025

WANAWAKE, WASICHANA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA AJIRA KATIKA SEKTA YA BAHARI

  

Na Mwandishi Wetu, Iringa

Wanawake na Wasichana wameaswa kutumia fursa za ajira zilizopo katia sekta ya bahari ikiwemo kuwa madereva wa meli, wahandisi na hata kutoa huduma za chakula na usafi ndani ya meli.

Wito huo umetolewa mjini Iringa leo na Mariam Mwayela, Afisa Mahusiano Mwandamizi wa Wakala wa Meli Tanzania wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake mjini Iringa yaliyoandaliwa na Sauti ya Haki Tanzania kuelekea kilele cha maadhimisho hayo Machi 8.

Mwayela amesema kumekuwa na mtazamo kwamba kazi za kwenye meli ni za wanaume tu jambo ambalo si la ukweli kwani hata mwanamke anaweza kuendesha meli, akawa mhandisi au kutoa huduma mbalimbali kama za chakula na usafi na kujipatia kipato.

Amewaasa watoto wa kike kuchukua kozi za usafiri majini ili waweza kupata ajira katika sekta hiyo muhimu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Sauti ya Haki Tanzania ambaye pia ni Makamu Rais wa TLS Wakili Laetitia Ntagazwa alisema kuwa wanawake bado wameendelea kupata changamoto nyingi zikiwemo vipigo, kuporwa mali, umaskini wa kiuchumi na migogoro ya mali.
Ni kwa mantiki hiyo ndiyo maana maadhimisho hayo yalijumuisha mawakili nane ambao walikuwepo hapo kutoa elimu juu ya masuala mbalimbali yakiwemo sheria ya ardhi, mirathi, ndoa, haki za watoto na namna ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia.

Sambamba na hilo, maadhimisho hayo yalijumuisha uchangiaji wa damu salama ambapo pia wanachama watakwenda kutembelea wafungwa na kutoa misaada ya kibinadamu.

Maadhimisho hayo yamewakutanisha washiriki 160 wakiwemo wanawake wa vikundi, viongozi wa serikali za mitaa, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, na wanasheria.

Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ni Tarehe 8 Machi.

Maadhimisho hayo kwa upande wa Iringa yemefadhiliwa na Wakala wa Meli Tanzania na ASAS.


Mkurugenzi wa Sauti ya Haki Tanzania na Makamu wa Rais wa TLS wakili Laetitia Ntagazwa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages