Breaking

Tuesday, 11 March 2025

WAFANYABIASHARA WA SOKO LA KARIAKOO WAPEWA SEMINA

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM.

SHIRIKA la Masoko ya Kariakoo limeendesha Semina ya Siku mbili kwa waliokuwa wafanyabiashara wa soko la Kariakoo ambao wanatarajiwa kurejeshwa ndani ya soko kufuatia kukamilika kwa mradi ujenzi na ukarabati wa soko.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Semina hiyo leo Machi 11,2025 Jijini Dar es Slaam, Afisa Uhusiano Mkuu wa Revocutus Kassimba amesema wamekutana na wafanyabiashara hao kwaajili ya kuwapitisha kwenye mahitaji ya msingi ambayo wanatakiwa kuanza kuyafanya kabla ya kurudi sokoni.

Amesema kupitia semina hiyo wamewafundisha matumzi ya mfumo wa kieletroniki wa TAUSI ambao utatumika kwaajili ya kusajili wafanyabiashara kwenye mfumo na kutoa hati za malipo.

Aidha amesema kupitia ushirikiano wa wadau wao TRA, Mabenki, Jeshi la Zimamoto pamoja na wawakilishi wa wafanyabiashara wamekutana nao kuwapa elimu ya majanga ili kuepuka ajali zingine.

Amesema pia wamekutana kuwakumbusha kuhusu sera ya upangishaji wa Shirika nini wanapaswa wafanye ili wasiingine kwenye mgogoro na Serikali.

"Sera yetu ya upangishaji inasema, mtu mmoja kwa eneo moja na huyu mfanyabiashara atakapopewa eneo la biashara ndani ya soko la kariakoo hatapaswa kulipangisha kwa mtu mwingine". Amesema

Pamoja na hayo amewapongeza wafanyabiashara hao kutoa muda wao na kushiriki katika mafunzo hayo muhimu katika uendeshaji wa biashara zao.

Kwa upande wake Afisa TEHAMA wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, Emmanuel Mjunguli amesema mfumo wa TAUSI ni mfumo rafiki sana na unawatengenezea fursa na kuwaondolea changamoto mbalimbali wafanyabiashara.

Amesema mfumo huo umekuja na usajili wa kutumia kitambulisho cha NIDA ambapo mfanyabiashara anakuwa na taarifa zake kamili ndani ya mfumo.

"Niwatoe hofu wafanyabiashara wote waweze kujiunga na mfumo huu, hakuna vigezo vilivyowekwa kwaajili ya kumuangusha mfanyabiashara yoyote. Mfumo huu tayari umeshaanza kutumika miaka miwili nyuma na halmashauri mbalimbali na hakuna changamoto yoyote waliyoipata". Amesema

Naye Mfanyabiashara Ruth Myonga amesema kupitia semina hiyo wanakwenda kupata uelewa kuhusu uendeshaji wa biashara zao na kuweza kunufaika kiuchumi.

Ramadhani Mtengule ambaye ni Mfanyabiashara wa Kariakoo amesema mfumo wa TAUSI unawapa matumaini kwasababu walikuwa wamekaa kimya na hawajui kinachoendelea, hivyo wanavyozidi kuwaelimisha ndo wanapata mwanga wa matumaini ya kurudi katika biashara zao.

Hata hivyo ameuomba uongozi kuhusu mafunzo hayo yawe endelevu ili wafanyabaishara hao waendelee kupata uelewa mkubwa namna ya uendeshaji wa biashara zao katika soko la Kariakoo.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages