Mwongozo wa elimu ya saikolojia kwa wagonjwa wa skizofrenia na ndugu zao kutambuliwa rasmi kwenye miongozo ya tiba ili kuelimisha Jamii kuhusiana na afya ya akili.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa hospital ya taifa ya afya ya akili Dr. Paul S Lawala wakati wa Kikao kazi cha na wadau wa Tafiti ya KUPAA kwaajili ya uboreshwaji wa huduma na elimu ya afya ya akili kwa wagonjwa na zao.
Amesema uwepo wa muongozo wa huduma za wagonjwa wa skizofrenia utasaidia kutambua wagonjwa pamoja na familia zao na kusaidia watu wanaoumwa au watakaoumwa badaye.
“Utafiti huu utasaidia namna gani huduma hizi za wagonjwa wa skizofrenia pamoja na familia zao zinaweza zikapata kutambuliwa rasmi kwenye miongozo ya tiba na kusadia watu ambao wanaumwa na wengine ambao pengine watakuja kuumwa,”amesema Dkt. Lawala
Aidha, amesema kwenye nchi zilizoendelea kuna miongozo ambayo inaota kama afua, muongozo wa saikolojia kwa familia na wagonjwa sasa kwa wanaojua kuwa miongozo inasaidia kusema nini kifanyike na kwa utaratibu gani kwa kundi fulani la wagonjwa.
Amesema, kwenye afya ya akili taarifa zilizopo na imani zilizopo na utambuzi uliopo ni mdogo sana, hivyo katika kazi nyingine ambayo itawafaa kufanya ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu tatizo la afya ya akili kwa jamii.
“Kwahiyo kitu tunachokitegemea na kukichukua kwenu kwa mazingira yetu hatutaweza kuchukua kila kitu cha kule kwa wenzetu kwenye miongozo yao bali tutengeneze miongozo yetu ambayo iasaidia kutambua wagonjwa pamoja na familia zao ili kusaidia wanaoumwa na wale watakao umwa” ameeleza Dkt. Lawala.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Afya ya Akili na Mkuu wa Kitengo cha Utafiti kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dkt. Innocent Rwiza Mwombeki amesema kuwa utafiti huo utafanyika kwa Mikoa ya Dar Es Salaam, Kilimanjaro, Mbeya na Dodoma kwa lengo la kusaidia kundi la wagonjwa na ndugu zao kupunguza makali ya ugonjwa wa skizofrenia nchini.
“Tupo katika mwaka wa kwanza wa utafiti na utafiti huu ni wa miaka mitano, ambapo tumepokea maoni ya wadau ambao ni Wagonjwa wa skizofrenia, waganga Wakuu wa Mikoa na wilaya na ndugu wa wagonjwa hao”, ameeleza Dkt. Mwombeki
Dkt. Mwombeki amesema kuwa Matokeo ya utafiti yakiwa chanya watahakikisha wanaweka miongozo imara ya ugonjwa wa skizofrenia ili kuboresha Huduma za wagonjwa hao bila kulazwa hospitali na afua hiyo inaendana na matumizi ya dawa mgonjwa akiwa nyumbani akiuguzwa na ndugu zake.