Breaking

Monday, 31 March 2025

TEA NA WFP WAHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA


Mnamo tarehe 27 Machi 2025, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) iliungana na Ubalozi wa Uingereza pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa – Mpango wa Chakula Duniani (World Food Programme - WFP) katika kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia mashuleni.

Uhamasishaji huu ulifanyika kupitia warsha maalum iliyowakutanisha walimu wakuu, wapishi, na walimu wa lishe kutoka shule 50 za Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam. 

Warsha hiyo iliyofanyika katika Shule ya Msingi Liwati, ililenga shule zinazotarajiwa kufadhiliwa na WFP ili kuanza kutumia nishati safi ya kupikia.

Katika warsha hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi ya Elimu wa TEA, Bw. Masozi Nyirenda, aliambatana na Kaimu Meneja wa Utafutaji Rasilimali na Hamasa wa TEA, Dkt. George Mofulu. 

Bw. Nyirenda aliwaeleza wadau wa nishati safi ya kupikia kuwa TEA iko mbioni kutafuta zaidi ya Shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwenye takriban shule 500 za sekondari nchini ndani ya kipindi cha miaka mitano. 

Aidha, alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wadau kushirikiana na TEA kwa kufadhili mradi huo ili kutunza mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji.

Kwa upande mwingine, Balozi wa Uingereza nchini, Bi. Marianne Young pamoja na Mwakilishi wa WFP nchini, Bw. Ronald Tran Ba Huy, walipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zake za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia mashuleni na wakaahidi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages