Breaking

Sunday, 9 March 2025

SIKU YA WANAWAKE DUNIANI : UDSM YATEMBELEA NA KUTOA MSAADA GEREZA LA SEGEREA


Katika kuadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake kwa mwaka 2025, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeadhimisha siku hii kwa kutekeleza jukumu lake la kuhudumia jamii kwa kutoa misaada kwa makundi yenye uhitaji.

Katika zoezi hilo, wanawake wa UDSM wakiongozwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Jinsia, Dkt. Lulu Mahai, wametembelea Gereza la Mahabusu la Segerea, Kituo cha Wazee Nunge na Kambi ya Watoto Kurasini na kutoa misaada ya mahitaji muhimu kwa wanawake wafungwa, wazee na watoto.

Katika Gereza la Segerea, msaada huo ulilenga kuboresha ustawi wa wanawake waliopo gerezani pamoja na watoto wao.

Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Hamida M. Matimba, aliishukuru UDSM kwa mchango wake, akisisitiza umuhimu wa elimu ya sheria ili kuwasaidia wanawake kuepuka makosa yanayoweza kuwapeleka kwenye mfumo wa uhalifu.

Katika Kambi ya Watoto Kurasini ambayo ina jumla ya watoto 68, wakiwemo wasichana 12, wanawake wa UDSM waliwakabidhi watoto hao msaada wa mahitaji ya kila siku.

Mlezi wa kituo hicho, Bw. Twaha Kibalula, aliwashukuru kwa upendo wao, akibainisha kuwa ujio wao si tu msaada wa vitu bali pia ni faraja kwa watoto hao.

Kwa upande wa Kituo cha Wazee Nunge, kilichopo chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, wanawake wa UDSM walitoa misaada mbalimbali ili kuboresha maisha ya wazee hao.

Dhamira ya UDSM kwa Jamii

Akizungumza katika hafla hizo, Dkt. Lulu Mahai alisisitiza kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hakifundishi tu bali pia kinajikita katika kufanya tafiti na kuhudumia jamii.

“Tunahakikisha kuwa tunachangia maendeleo ya jamii kwa vitendo, kwa sababu jamii salama ni jamii inayojali na kusaidia makundi yenye uhitaji,” alisema.

Kwa misaada hii, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinaendelea kuonesha dhamira yake ya kuleta mabadiliko chanya kwa jamii kwa vitendo, kuhakikisha kuwa hata wanawake waliopo katika mazingira magumu wanapata msaada wa msingi.

Mwaka huu kauli mbiu ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake, ambayo huadhimishwa kila tarehe 8 mwezi Machi, ni “Kwa Wanawake na Wasichana Wote: Haki. Usawa. Uwezeshaji”.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages