Na Rose Ngunangwa - Dar es salaam
Serikali imeandaa mwongozo kwa wanamuziki ili kulinda maadili ya kitanzania pale wanapotengeneza maudhui na picha mjongeo katika kazi zao.
Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa wakati akifungua warsha ya kuorodhesha urithi wa utamaduni usioshikika ili kuulinda muziki wa Singeli.
Msigwa alisema kwamba katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na maoni kinzani kuhusu Singeli kuorodheshwa kwenye urithi wa utamaduni usioshikika wa UNESCO huku baadhi wakitoa sababu za muziki huo kukosa maadili.
“ Hatuwezi tukasema muziki wote wa Singeli ni mbaya kwa sababu tu wimbo mmoja au watu wachache wanakiuka maadili. Kinachotakiwa ni kuhakikisha kuwa tunawawajibisha wale ambao hawazingatii maadili ili kulinda mila na utamaduni wa kitanzania,” alisema Msigwa.
Alisisitiza kuwa ni vema wanamuziki wakajipima pale wanapoandaa kazi zao na kutafakari iwapo wanaweza kukaa na kuangalia na mama zao kabla ya kurusha.
Kwa mujibu wa Msigwa, Wizara yake ipo macho na pale inapoona muziki haukidhi maadili huutoa mara moja na kuwasiliana na Baraza la Sanaa la Tanzania ambalo huwaita wasanii na kuwaonya.
Kwa upande wake, mwanamuziki wa Singeli alimaarufu kama Msaga Sumu ametoa shukrani kwa Serikali na UNESCO kwa kuona umuhimu wa kuutangaza muziki huo duniani kwani wamekuwa wakiimba bila kujua kwamba ipo siku kazi zao zitakwenda kimataifa.
Singeli ni zaidi ya muziki kwani ni urithi wa utamaduni ulio hai unaoakisi ubunifu na ustahimilivu wa watanzania.
Neno Singeli linatokana na mmoja wa wachezaji wa muziki huo ajulikanaye kama Kisingeli ambapo wanamuziki hao walitoa neno Ki ili kutodogoresha na kuuita singeli.
Muziki huo unapendwa na watu wa rika na jinsi zote ambapo lugha inayotumika ni Kiswahili ambapo ina mafunzo na ucheshi ndani yake.
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Ofisi ya Kanda ya Afrika Mashariki ya UNESCO pamoja na ofisi ya UNESCO Dar es Salaam wameandaa warsha ya siku mbili ili kukuza uwezo wa nchi katika kuandaa faili la uteuzi wa orodha ya UNESCO ya urithi wa utamaduni usioshikika huku kipaumbele kikiwa ni muziki wa Singeli.



