Breaking

Monday, 24 March 2025

SERIKALI KUUKUZA NA KUULINDA MUZIKI WA SINGELI


Na Rose Ngunangwa - Dar es salaam

Serikali imeahidi kufanya jitihada ya kuukuza na kuulinda muziki wa Singeli ikiwemo kuuorodhesha kwenye orodha ya UNESCO ya urithi wa utamaduni usioshikika duniani ili kukuza lugha ya Kiswahili na Utalii wa Utamaduni.

Ahadi hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,Gerson Msigwa wakati akifungua warsha ya kuorodhesha urithi wa utamaduni usioshikika ili kuulinda muziki wa Singeli.

Msigwa alisema katika miaka ya hivi karibuni muziki wa singeli umetoka kwenye kutoa burudani hadi kuelimisha jamii na kusema utafiti unaonyesha kuwa muziki huu ni wa kipekee kwani hakuna nchi yoyote duniani inayopiga.

Kwa upande wake, Mkuu wa Ofisi ya UNESCO nchini, Michel Toto aliulezea muziki wa singeli kama moja ya simulizi zenye nguvu zinazostahili kusherehekewa, kulindwa na kukuzwa kwani unaunganisha watu na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Singeli ni zaidi ya muziki kwani ni urithi wa utamaduni ulio hai unaoakisi ubunifu na ustahimilivu wa watanzania.

Neno Singeli linatokana na mmoja wa wachezaji wa muziki huo ajulikanae kama Kisingeli ambapo wanamuziki hao walitoa neno Ki ili kutodogoresha na kuuita singeli.

Muziki huo unapendwa na watu wa rika na jinsi zote ambapo huleta amsha amsha pale unapopigwa.

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Ofisi ya Kanda ya Afrika Mashariki ya UNESCO pamoja na ofisi ya UNESCO Dar es Salaam wameandaa warsha ya siku mbili ili kukuza uwezo wa nchi katika kuandaa faili la uteuzi wa orodha ya UNESCO ya urithi wa utamaduni usioshikika huku kipaumbele kikiwa ni muziki wa Singeli.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages