Breaking

Saturday, 15 March 2025

PURA yaongeza jitihada kufungamanisha sekta ya mafuta na gesi na sekta ya elimu nchini

Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imeendelea kutekeleza programu mbalimbali zinazolenga kufungamanisha sekta ya mafuta na gesi asilia na sekta ya elimu nchini.

Miongoni mwa programu hizo ni pamoja na kutoa fursa kwa wadau wa sekta ya elimu kutembelea miundombinu ya uzalishaji na uchakataji wa gesi asilia iliyopo katika mikoa inayozalisha gesi asilia nchini kwa lengo la kuongeza uelewa wa wadau hao muhimu.

Katika hili, tarehe 14 Machi 2025, PURA iliwezesha ziara ya wadau kutoka vyuo vya elimu ya juu, vyuo vya elimu ya kati na vyuo vya ufundi nchini kutembelea mitambo ya kuzalisha na kuchakata gesi asilia iliyopo Mkoani Mtwara.

Ziara hiyo pia ilihusisha wadau kutoka mamlaka zinazohusika na udhibiti wa ubora wa elimu ikiwemo Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET)

Kupitia ziara hiyo, wadau hao walipata fursa ya kutembelea mitambo ya kuzalisha na kuchakata gesi asilia iliyopo Mnazi Bay inayoendeshwa na kampuni ya Maurel et Prom na mitambo ya kuchakata gesi asilia iliyopo eneo la Madimba inayoendeshwa na GASCO ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Pamoja na maeneo hayo, wadau hao walipata fursa ya kutembelea Chuo cha Ualimu Mtwara (Kawaida) kwa lengo la kuona namna ambavyo matumizi ya gesi asilia yameleta mapinduzi katika chuo hicho baada ya kuacha matumizi ya kuni kama chanzo cha nishati wakati wa kupika na kuhamia katika matumizi ya gesi asilia.

Wakizungumza wakati wa ziara hiyo, wawakilishi wa wadau hao akiwemo Dkt. Malehe Cosmas Setta ambaye ni Mthibiti Ubora Mkuu kutoka TCU, Bw. John Ndega ambaye ni Meneja anayehusika na utafiti ndani ya VETA na Dkt. Adela Syikilili ambaye ni mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wamesema ziara hiyo, pamoja na kuongeza uelewa, imewasaidia kupata picha halisi ya kiwango cha utaalamu kinachohitajika katika tasnia ya mafuta na gesi asilia jambo ambalo litaongeza tija wakati wa maandalizi ya mitaala inayohusiana na masuala ya mafuta na gesi.

Kwa upande wake, mwakilishi kutoka PURA Bw. Musa Ryoba alisema kuwa ziara hiyo ni mwendelezo wa jitihada za PURA katika kuhakikisha kuwa sekta ya mafuta na gesi asilia nchini inafungamanishwa na sekta nyingine za kiuchumi ikiwemo elimu kwa kuwa ili sekta ya mafuta na gesi iwe na mchango mkubwa katika uchumi ni lazima sekta hiyo ifungamanishwe na sekta zingine hususan sekta za kimkakati.
Mhandisi Haruna Mchessu kutoka kampuni ya Maurel et Prom akielezea jambo kwa wadau wa elimu wakati ziara iliyoandaliwa na PURA kwa lengo la kuongeza uelewa wa wadau hao kuhusiana na masuala ya uzalishaji na uchakataji wa gesi asilia katika eneo la Mnazi Bay Mkoani Mtwara.
Wadau wa masuala ya elimu katika picha ya pamoja na wataalamu kutoka PURA na  Maurel et Prom wakati ziara iliyoandaliwa na PURA kwa lengo la kuongeza uelewa wa wadau hao kuhusiana na masuala ya uzalishaji na uchakataji wa gesi asilia Mkoani Mtwara.
Mhandisi Haruna Mchessu kutoka kampuni ya Maurel et Prom akielezea jambo kwa sehemu ya wadau wa elimu wakati ziara iliyoandaliwa na PURA kwa lengo la kuongeza uelewa wa wadau hao kuhusiana na masuala ya uzalishaji na uchakataji wa gesi asilia katika eneo la Mnazi Bay Mkoani Mtwara.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages