Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Tanzania (PSSSF) umeendelea kuimarisha mchango wake katika kukuza uchumi wa taifa kwa kuboresha uwekezaji wake, na kufanikiwa kuongeza kiwango cha maendeleo kutoka asilimia 22 mwaka 2023 hadi asilimia 36 mwaka 2024/2025.
Lengo hili linakaribia kufikiwa kwa kiwango cha asilimia 40 kilichopendekezwa kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa Tanzania.
Hayo yamesemwa leo, Machi 14, 2025, na Mwanasheria Mkuu wa PSSSF, Valentino Maganga, alipokuwa akitoa taarifa kwenye Mkutano wa Wadau wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA-Tan) 2025, uliofanyika Jijini Dodoma.
Maganga amesema mfuko huo umefanikiwa kuongeza thamani ya uwekezaji kutoka trilioni 6 hadi trilioni 10, hatua inayochochea maendeleo ya uchumi wa nchi.
Vilevile, ameongeza kuwa dhamana za uwekezaji zilizopo kwenye taasisi za kifedha, kama vile benki na majumba, zenye thamani ya Shilingi Trilioni 9, zinachangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza pato la taifa na ukuaji wa uchumi.
Aidha, amesema PSSSF inalipa pensheni kwa wastafu kila mwezi kiasi cha Shilingi Bilioni 70, na kwa mwaka ni zaidi ya Shilingi Bilioni 800, fedha ambazo huchochea shughuli za uchumi na kusaidia katika uwekezaji unaoingizia mapato Serikali.
Picha : MATUKIO YANAYOENDELEA MKUTANO 'MISA - WADAU SUMMIT 2025'