Na Mwandishi Wetu
Tume ya Utumishi wa Umma imetoa rai kwa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuwekeza zaidi katika kutoa elimu ya masuala ya usalama na afya kwa waajiri na wafanyakazi wote nchini hususan katika sekta ya umma ili kuwawezesha kutambua vihatarishi vya magonjwa na ajali mahali pa kazi na hivyo kuchukua tahadhari za kujilinda.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Hamisa Kalombola, wakati wa ziara ya Tume hiyo katika Ofisi za OSHA Dar es Salaam Machi 04, 2025 akiwa ameambatana na Katibu wa Tume, Makamishna na Watendaji mbalimbali wa Tume hiyo.
Lengo la ziara hiyo ilikuwa na kujifunza kuhusu usimamizi wa masuala ya usalama na afya katika sekta ya umma ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Mhe. George Simbachawene alilolitoa Novemba 16, 2024 alipofanya ziara OSHA ambapo aliitaka Tume hiyo kutembelea Taasisi ya OSHA kwa minajili ya kupata ufahamu wa masuala husika.
Mheshimiwa Kalombola amesema jukumu kuu la Tume ni kusimamia utekelezaji wa Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma katika Sekta ya Umma ambapo katika kipindi cha hivi karibuni masuala ya usalama na afya yamejumuishwa katika mwongozo wa ukaguzi unaofanywa na Tume.
“Uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya katika Taasisi za Umma ni miongoni mwa masuala ambayo Tume inatarajia kuanza kuyafanyia ukaguzi hivyo imetulazimu kuja OSHA kujifunza ili tuweze kufanya kazi yetu ipasavyo,” ameeleza Mheshimiwa Kalombola na kuongeza:
“Sambamba na kutoa mafunzo kwa waajiri na wafanyakazi nitoe rai kwenu OSHA kuhakikisha kwamba Wakaguzi wa Tume wanapatiwa mafunzo mahsusi ya usalama na afya pamoja na kushirikiana nao kuboresha madodoso yatakayotumika kufanya ukaguzi kwani usalama na afya si hitaji la kisheria tu bali ni wajibu wa kimaadili kwa waajiri.”
Akizungumza baada ya kikao baina ya Tume na OSHA, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema katika kikao hicho wameipitisha Tume katika Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na muundo wa OSHA na majukumu yake ya msingi katika kuisimamia utekelezaji wa sheria tajwa.
Bi Mwenda, ameongeza kuwa Menejiementi ya OSHA na ujumbe wa Tume wamefanya majadiliano ya kina kuhusiana na namna ambavyo watashirikiana na Tume katika kuiwezesha kufuatilia uzingatiaji masuala ya usalama na afya katika sekta ya umma.
“Niwaombe wakuu wenzangu wa Taasisi za umma kutekeleza maelekezo ya serikali yanayotutaka kusajili maeneo ya kazi OSHA na kuhakikisha kunakuwa na uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya kwani kinyume na hivyo, Taasisi zao hazitakidhi viwango vya ukaguzi wa utekelezaji wa sheria za utumishi wa umma unaofanywa na Tume ya Utumishi wa Umma,” alieleza Mtendaji Mkuu wa OSHA.
OSHA ni Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) yenye dhamana ya kulinda nguvukazi ya Taifa kupitia usimamizi wa Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003. Usimamizi huu hufanyika kupitia usajili wa maeneo ya kazi na ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya katika maeneo husika ili kuhakikisha kwamba inakidhi viwango stahiki.

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu Hamisa H. Kalombola, akifuatilia mawasilisho kuhusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi, wakati wa ziara yake katika Ofisi za Wakala Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Machi 4, 2025 Jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akiwasilisha mada kuhusu Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, muundo wa Taasisi ya OSHA pamoja na majukumu yake ya msingi wakati wa ziara ya Tume ya Utumishi wa Umma ilipotembelea Ofisi za OSHA, Machi 4, 2025 Jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda akimwelekeza Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu Hamisa H. Kalombola namna ya kutumia kiti cha igonomia wakati wa ziara ya Tume hiyo katika Ofisi za OSHA, Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Usalama na Afya wa OSHA, Dkt. Jerome Materu, akijibu baadhi ya hoja za wajumbe wa kikao baina na OSHA na Tume ya Utumishi kwa Umma ilipofanya ziara katiaka Ofisi za OSHA Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Mafunzo, Tafiti, Takwimu na Uhamasishaji, Bw. Joshua Matiko akijibu baadhi ya hoja za wajumbe wa kikao baina na OSHA na Tume ya Utumishi kwa Umma ilipofanya ziara katika Ofisi za OSHA Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wajumbe wa kikao baina ya OSHA na Tume ya Utumishi wa Umma wakifuatilia kwa ukaribu mawasilisho mbalimbali kuhusu OSHA na majukumu yake walipo fanya zira katika Ofisi za OSHA Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu Hamisa H. Kalombola (katikati), akiwa kwenye picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda (wapili kulia). Wengine ni Makamishna na Watendaji wa Tume ya Utumishi wa Umma wakiwemo baadhi ya watumishi wa OSHA.