Na Samir Salum - Darubini ya Ulimwengu
"Dunia ni nukta ya buluu iliyo mbali sana, lakini sisi ni watu wa hapa. Hakuna pa kukimbilia. Ni juu yetu kuitunza." – Carl Sagan
Mwanadamu amekuwa akiangalia angani kwa maelfu ya miaka, akijiuliza maswali yasiyo na majibu. Lakini kulikuwa na mtu mmoja aliyefanya anga za juu kuwa hai machoni mwa wengi, Carl Sagan, Mwanasayansi huyu hakutosheka tu na kutazama nyota, alihamasisha ulimwengu mzima kuelewa uzuri wa sayansi kwa lugha rahisi na yenye mvuto. Alikuwa daraja kati ya ulimwengu wa kawaida na ulimwengu wa nyota.
Carl Sagan alizaliwa tarehe 9 Novemba 1934, huko New York, Marekani. Tangu akiwa mdogo, alikuwa na hamu kubwa ya kujua kuhusu sayari, nyota, na uwezekano wa maisha nje ya dunia yetu. Alipenda vitabu vya sayansi na kila mara alikuwa na swali moja kubwa: Je, tuko peke yetu katika ulimwengu huu mkubwa?
Katika maisha yake, Sagan alifanya mambo makubwa ikiwemo kuhusika katika miradi ya kutuma vyombo vya anga kama Voyager 1 na 2, ambavyo vinasafiri mbali na mfumo wetu wa jua.
Alisaidia kuelewa hali ya sayari kama Venus na Mars, akigundua kuwa Venus ina joto kali kutokana na gesi za chafu na pia alibuni ujumbe wa dhahabu (Golden Record) uliopelekwa angani, kama salamu kwa viumbe wa mbali iwapo wangeupata siku moja.
Lakini kubwa zaidi, aliifanya sayansi kuwa rahisi kueleweka kwa kila mtu. Kupitia kitabu chake Cosmos na kipindi maarufu cha televisheni chenye jina hilo hilo, aliwafanya watu wengi kupenda anga za juu.
Sagan hakutumia namba na fomula pekee, alitumia maneno yenye nguvu na hisia. Alisema, "Tuko hapa kwa muda mfupi sana katika historia ya ulimwengu, lakini tunaweza kutumia muda huo kuelewa sehemu yetu katika sayari na anga lote."
Alisisitiza umuhimu wa kushangazwa na sayansi, si kwa sababu ni kazi, bali kwa sababu sayansi ni njia ya kuona uzuri wa ulimwengu kwa macho mapya.
Carl Sagan alifariki tarehe 20 Desemba 1996, lakini kazi yake bado inaishi. Leo, vipindi vya sayansi vinaendelea kufuata nyayo zake, na mamilioni ya watu bado wanapenda anga za juu kwa sababu ya juhudi zake.
Aliwaambia wanadamu wasiangazie tu ardhi wanapopita, bali waangalie juu, waangalie nyota, na waulize maswali.
Carl Sagan alikuwa zaidi ya mwanasayansi, alikuwa mwalimu, mshairi wa sayansi, na daraja kati ya watu wa kawaida na ulimwengu wa anga za juu. Alitufanya tuamini kuwa kila mtu ana nafasi yake miongoni mwa nyota.
Mwisho
References
1. NASA - Carl Sagan’s Contributions to Space Exploration: https://www.nasa.gov
2. The Planetary Society - The Legacy of Carl Sagan: https://www.planetary.org
3. Cosmos: A Personal Voyage - History and Impact: https://www.cosmos.com