
Menejimenti ya VETA ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA. Anthony Kasore, leo, tarehe 7 Machi 2025 imetembelea kiwanda cha Emirate Alluminium Profile kilichopo Tegeta jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza na kupata uzoefu kuhusu namna ufundi wa Aluminiamu unavyofundishwa sehemu ya kazi.
Ziara ililenga pia kuona namna ya kuanzisha ushirikiano kati ya VETA na Emirate Alluminium Profile ili kuwezesha wanafunzi wanaosoma katika vyuo vya VETA kupata ujuzi zaidi kuhusiana na ufundi wa Aluminiamu kupitia mafunzo ya mahala pa kazi. Akizungumza katika ziara hiyo Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA. Anthony Kasore, amesema wamebaini shughuli za ufundi zinazofanywa katika kampuni hiyo zinaakisi Mitaala ya VETA, ambapo wanafunzi wa fani ya Useremala wanafundishwa masuala ya utengenezaji wa Aluminiamu.
CPA Kasore amesema kiwanda hicho kina mafundi waliobobea wenye uzoefu ambao VETA itawatumia kutufundisha na kufundisha katika vyuo vyake.
"Sisi VETA kwa kukutana na Emirates Alluminium Profile tunaenda kuwa na ushirikiano ambao utawezesha kutoa huduma na kuwezesha watu kwenda kupata ujuzi utakaowasaidia kujiajiri na kuajiriwa katika viwanda mbalimbali nchini," amesema CPA Kasore.
Aidha, CPA Kasore amesema kupitia ziara hiyo wameona kuna haja ya kutenganisha ufundi wa Aluminiamu na Useremala, ili kila moja iweze kujitegemea, hivyo kuzalisha vijana waliobobea kwenye ufundi wa Aluminiamu ambao una fursa nyingi kwa sasa.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Emirate Alluminium Profile, Ndugu Deogratius Marandu amewataka vijana kuwekeza katika kufanya kazi kwa kutumia mikono na sio kutumia ujanja ujanja ili kufanikiwa na hivyo kuiomba VETA kuendelea na kazi ya kuwaanda vijana ili waweze kuajirika na kujiajiri na kuchangia katika maendeleo ya jamii zao na Taifa.
"Mimi nina imani sana na VETA hasa katika kuwanoa vijana naamini tunaenda kushuhudia mabadiliko mbalimbali katika masuala ya Ufundi stadi na tunaenda kuwapata wataalamu watakaoenda kufanya kazi kwa ufanisi," amesema. Kiwanda cha Emirate Alluminium Profile kinajihusisha na uagizaji na uuzaji wa Aluminiamu, vioo, pamoja na mipira kwa ajili ya kutengenezea madirisha na milango ya Aluminiamu.
















