Breaking

Tuesday, 18 March 2025

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YAHITIMISHA ZIARA YA UKAGUZI WA MIRADI YA UMEME MKOANI NJOMBE

18 Machi,2026, Njombe

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imekamilisha ziara yake ya siku tatu mkoani Njombe kwa kukagua utekelezaji wa miradi ya Nishati Vijijini (REA) inayotekelezwa na serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Kwa upande wa REA ziara hiyo imehitimishwa katika kijiji cha Welela, Jimbo la Lupembe, ambapo kamati hiyo imepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali kuhakikisha umeme unawafikia wananchi wa vijijini kwa kasi inayostahili.

Akizungumza wakati wa hitimisho la ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Dkt. David Mathayo, alisema kamati yake imeridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo, lakini akasisitiza kuwa bado kuna haja ya kuongeza kasi ili kufanikisha lengo la Serikali la kuhakikisha vitongoji vyote nchini vinaunganishwa na gridi ya taifa kwa wakati.

"Tumetembelea vijiji mbalimbali, vikiwemo Mang’oto, Lwangu na Welela, tumeona maendeleo mazuri ya usambazaji wa umeme wa REA. Hata hivyo, bado tunasisitiza kuongeza kasi ya utekelezaji ili wananchi wote wanufaike na huduma hii muhimu," alisema Dkt. Mathayo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha changamoto zote za umeme vijijini zinatatuliwa kwa haraka ili kuboresha maisha ya wananchi.

"Serikali inatambua umuhimu wa umeme kwa maendeleo ya wananchi, hususan katika sekta za elimu, afya, na biashara. Tutaendelea kuweka msukumo ili kuhakikisha vitongoji vyote vinapata umeme kwa wakati, na kwa hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi," alisema Mhe. Kapinga.

Wananchi wa Kijiji cha Welela, Jimbo la Lupembe, wameeleza furaha yao kwa kupatiwa umeme kupitia Miradi ya umeme Vijijini inayoendelea kutekelezwa na REA, wakisema kuwa hatua hiyo imewasaidia kuondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma muhimu, ikiwemo mashine za kusaga nafaka.

Wakizungumza mbele ya Kamati ya Bunge, wananchi hao walieleza kuwa umeme huo umeleta mabadiliko makubwa katika maisha yao ikiwa ni pamoja na kuwaongezea kipato kwakua wanautumia kwa shughuli za kiuchumi.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Oliva Kaduma, alisema kuwa uwepo wa umeme umeimarisha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa urahisi, hali inayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalumu wa Kata ya Mtwango, Rhoda Wanderage, aliishukuru Serikali kwa kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, akisema kuwa hatua hiyo imesaidia kutatua changamoto nyingi za kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo. 

Pia, alitoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo inayowanufaisha wananchi wa vijijini.

"Zamani tulilazimika kutembea umbali mrefu kusaga nafaka au kupata huduma nyingine zinazotegemea umeme, lakini sasa kila kitu kipo karibu. Tunamshukuru sana Rais Samia kwa juhudi hizi," alisema Wanderage.

Naye Mkurugenzi wa umeme Vijijini kutoka wakala wa Nishati vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu, alieleza kuwa jumla ya shilingi bilioni 81.6 zinatumika kutekeleza miradi ya usambazaji wa umeme vijijini mkoani Njombe. 

Alibainisha kuwa miradi hiyo ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kuhakikisha vijiji vyote vinaunganishwa na gridi ya taifa, huku sehemu kubwa ya miradi hiyo ikiwa imekamilika ndani ya muda uliopangwa.

"Tunahakikisha kuwa vitongoji vyote vilivyoainishwa vinapata umeme kwa wakati. Pia, tupo katika hatua za mwisho za kutangaza Zabuni mpya ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme vitongojini," alisema Mhandisi Olotu.

Ziara hiyo kwa upande miradi ya REA imehitimishwa kwa Kamati ya Bunge kupokea taarifa rasmi ya utekelezaji wa miradi ya umeme mkoani Njombe ambapo miradi inayotekelezwa na REA Mkoani Njombe inagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 81.6
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages