Breaking

Monday, 17 March 2025

Kamati ya Bunge yaridhishwa na Utekelezaji wa Miradi ya Ujenzi UDSM

*Profesa Anangisye apongeza katika uwekezaji katika elimu

Na Mwandishi Wetu

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Elimu,Utamaduni na Sanaa imesema kuwa miradi ya ujenzi wa hosteli wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam utapunguza changamoto ya wanafunzi kukaa nje ya chuo.

Mabweni ya Chuo hicho hadi sasa yanalaza wanafunzi 11,115 ukilinganisha na wanafunzi 22,000 wanaohitaji malazi chuoni hapo.

Ujenzi wa kuongeza ghorofa katika Hosteli za Magufuli umegharimu zaidi ya Sh.Bilioni Tatu ambapo wanafunzi 576 wameingia mara baada ya kukamilika Mei 2024.

Akizungumza katika ziara ya Kamati hiyo katika Chuo hicho Mwenyekiti wa Kamati hiyo Husna Sekiboko amesema kamati hiyo imeridhishwa na mradi wa hosteli na kutaka majengo hayo kutunzwa.

Sekiboko amesema kuwa baadhi ya wanafunzi wakiwa mitaani wanakabiliwa na changamoto zinazofanya baadhi yao kuingia katika makundi yanayofanya wasiendelee na masomo.

Hata hivyo amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeweka mkazo katika elimu kwa kuongeza bajeti yake.

Sekiboko amesema kuwa ujenzi huo wa hosteli katika Chuo hicho kuwa endelevu kutokana idadi ya wanafunzi wanaojiunga ikizidi kuongezeka kila mwaka.

Kamati hiyo pia imetembelea ujenzi wa Kituo cha Wanafunzi katika kampasi ya Mwalimu Julius Nyerere awamu ya pili wa Ghorofa unaogharimu sh.bilioni 13.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Sekiboko amesema ujenzi huo wa Kituo ulitokana na wazo Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuchangia waliosoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo fedha ambazo zilikusanywa wanafunzi waliopita ni Bilioni Nne.

Amesema kuwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan aliona mbali katika ujenzi huo ambao utakuwa ni jengo la mfano wa kuendelea kukitambulisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ukongwe wake.

Nae Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa William Anangisye amesema kuwa miradi ya ujenzi huo umesaidia kuongeza makazi ya malazi kwa wanafunzi na kuwapunguzia mzigo wa gharama ya huduma usafiri.

Amesema wanaishukuru Serikali kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni na kituo cha kisasa cha wanafunzi na kuahidi kusimamia katika kuyatunza.
Naibu wa Waziri wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga akitoa maelezo kwa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Elimu,Utamaduni na Sanaa ilipotembelea  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mwenyekiti  wa Kamati ya Kudumu ya Elimu ,Utamaduni na Sanaa Husna Sekiboko akiwa na wajumbe wa Kamati hiyo wakiangalia ubora vitanda katika mabweni mapya walipotembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Elimu ,Sayansi  na Teknolojia Omary Kipanga akipata maelezo kutoka Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam  Profesa William Anangisye wakati walipokuwa wakisubiri Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Elimu, Utamaduni  na Sanaa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages