Breaking

Friday, 7 March 2025

KAMATI YA BUNGE YA BAJETI YAPONGEZA BARRICK NORTH MARA KWA KUCHOCHEA MAENDELEO YA KIUCHUMI NA KIJAMII NCHINI

     

Wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya bajeti wakitembezwa katika maeneo mbalimbali ya mgodi wa North Mara
Wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya bajeti wakitembezwa katika maeneo mbalimbali ya mgodi wa North Mara
Wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya bajeti wakitembezwa katika maeneo mbalimbali ya mgodi wa North Mara
Wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya bajeti wakitembezwa katika maeneo mbalimbali ya mgodi wa North Mara
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Josephat Kandege akizungumza na wajumbe wa kamati , uongozi wa Mgodi wa Barrick North Mara na viongozi wa serikali Wakati wa ziara ya kamati hiyo leo mjini Nyamongo , Tarime vijijini
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko akitoa ufafanuzi baada ya wasilisho lake kuhusu shughuli za mgodi huo baada ya kamati ya kudumu ya bunge ya bajeti kufanya ziara kwenye mgodi huo
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya bajeti na wafanyakazi wa Barrick wakifuatilia mada zilizowasilishwa kwenye ziara hiyo.
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya bajeti na wafanyakazi wa Barrick wakifuatilia mada zilizowasilishwa kwenye ziara hiyo.

***

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Bajeti imefanya ziara kwenye Mgodi wa Barrick North Mara uliopo Nyamongo , Wilaya ya Tarime katika Mkoa wa Mara ili kujifunza na kujionea shughuli za utafiti, uchimbaji, uchenjuaji wa madini aina ya dhahabu katika Mgodi huo na imepongeza mgodi huo kwa kuendesha shughuli zake kwa tija na ufanisi mkubwa.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati Mbunge wa kalambo , Josephat Kandege amesema ziara hiyo imetoa fursa kwa wabunge wa kamati hiyo kujua changamoto zinazowakabili wawekezaji wa migodi hapa nchini ili kuweza kuzitafutia uvumbuzi wa kudumu.

“Mjipange katika siku za hivi karibuni mje Dodoma ili tuweze kukaaa chini na kuzungumza hizi changamoto za kodi, sheria mbalimbali ambazo ni kikwazo kwa wawekezaji kwenye sekta ya madini ili tuweze kuishauri Serikali kwa ufasaha zaidi ili ichukue hatua stahiki,”

“Lengo ni kuhakikisha sekta ya madini inaendelea kutoa mchango mkubwa kwenye pato la taifa letu na kuchochea ukuaji wa uchumi na utoaji wa ajira kwa watanzania,” amesema Kandege.

Kandege amesema kwa kutembelea mgodi huo wabunge wa kamati hiyo wana nafasi ya kujifunza jinsi shughuli za mgodi na namna ya watanzania wanavyoshirikishwa kwenye sekta ya uchimbaji wa madini hapa nchini.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Mgodi huo wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko amesema mgodi huo unaendelea kutekeleza kwa vitendo kanuni na sheria mbalimbali ikiwemo , Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) na Maudhui ya Ndani (Local content) ili kuhakikisha Watanzania wanaendelea kunufaika na uwepo wa migodi hapa nchini.

“Kwa sasa wafanyakazi kwenye migodi ya Barrick asilimia 96% ni watanzania na 13 % ni wanawake,Moja ya ajenda yetu ni uwezeshaji wa wanawake kushiriki kwenye sekta ya madini ili waendelee kutoa mchango wao kwenye ukuaji wa uchumi wa nchini,” amesema.

Amesema kwamba mgodi unaendelea kutoa mafunzo na kuwajengea uwezo wafanyakazi wake kwenye mgodi huo ili kuhakikisha kwamba watanzania wanaendelea kupata uwezo , kukuza ujuzi ili waweze kumudu nafasi mbalimbali na kuchukua nafasi za wageni ambao ni wataalamu.

Naye Mbunge wa jimbo la Musoma Mjini,Vedastus Mathayo amesema kwamba huko nyuma mgodi wa North Mara ulikuwa kwenye lawama nzito za uchafuaji wa mazingira na hasa vyanzo vya maji kwa kutititirisha maji yenye uchafu na sumu lakini tatizo hilo sasa limeshaghulikiwa.

“Nachukua fursa hii kuwapongeza uongozi wa mgodi wa Barrick North Mara kwa kuweza kuboresha utunzaji wa mazingira kwa kutengeneza miundombinu ya kisasa ya kuhifadhi maji yanayotokana na uchenjuaji wa dhahabu na kuweza kutunza mazingira,” ameongeza

Pia amepongeza mgodi kwa utekelezaji wa sera ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa ufanisi mkubwa kwa kuendelea kuchangia maendeleo katika sekta muhimu za maji, afya, elimu na ujenzi wa miundombinu ya Barabara ambayo ni kiungo muhimu kwa uchumi wa eneo husika.

“Kwa kweli mie nipo mbali kule Musoma Mjini lakini cheche za Uwajibikaji kwa Jamii nazipata maana wanatoa sio chini ya Tsh 7 billioni kwa mwaka hizi ni fedha nyingi na nachukua fursa hii kuwapongeza sana kwa kazi nzuri ya kuchangia maendeleo ya nchini yetu,” ameongeza.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages