Naibu
Waziri wa Viwanda na Biashara Mh. Exaud Kigahe, ameitaka Mamlaka ya Maabara ya
Mkemia Mkuu wa Serikali kuendelea kutoa elimu kwa Wajasiriamali ya namna bora
ya matumizi sahihi na salama ya kemikali katika bidhaa wanazozalisha ili
zisiweze kuleta madhara kwa jamii.
Naibu
Waziri Kigahe ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua maonesho ya
Viwanda na Biashara za Wanawake na Vijana Wajasiriamali Tanzania yaliyofanyika
katika Viwanja vya Mlimani City jijini Dar es Salaam.
“Nichukue
nafasi hii kuwashukuru sana TWCC kwa kuwaalika GCLA kuwa sehemu ya haya
maonesho, kwa sababu kama mnavyojua kwenye bidhaa zetu za Viwanda nyingi
zinatumia kemikali ambazo hazifai au kuzidisha ikawa hatari kwa afya za
watanzania. Hivyo, jukumu lenu ni kuendelea kutoa elimu kwa wajasiriamali hawa
ili wazalishe bidhaa zenye ubora lakini pia na usalama kwa walaji” alisema
Naibu Waziri Kigahe.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira Dkt. Shimo
Peter, amesema utekelezaji wa utoaji elimu tayari unafanyika na wanaendelea
kuwafikia wadau mbalimbali hapa nchini.
“Serikali
kupitia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali tumefungua Ofisi za Kanda
na katika hizo Ofisi za Kanda sita pamoja na madawati kwenye baadhi ya mikoa tumekuwa
tukitoa elimu kwa shughuli zetu zote tukiwashirikisha watoa huduma hao ambao ni
wazalishaji wa bidhaa, kuwapa elimu kuhusiana na bidhaa wanazozalisha,
kuhusiana na matumizi ya kemikali lakini pia huduma ya uchunguzi wa kimaabara
ambapo tumekuwa tukichukua sampili zao na kuzipima katika maaabara zetu na
kuwapa matokeo.
Lakini pia na kuwapa elimu stahiki ili
kuhakikisha kwamba bidhaa wanazozalisha zinakidhi viwango vya ubora wa ndani na
nje hata kama wapo katika mikoa mbalimbali au pembezoni mwa mji. Kwa hiyo yote
hii ni juhudi ya kuhakikisha kwamba elimu na huduma ya Mamlaka ya Maabara ya
Mkemia Mkuu wa Serikali imefika katika maeneo yote hapa nchini”. Alisema Dkt
Shimo.

