Breaking

Saturday, 8 February 2025

WATUMISHI MADINI WATAKIWA KUONGEZA BIDII KUFIKIA LENGO LA KUCHANGIA 10% PATO LA TAIFA



Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amewataka watendaji na watumishi wa Wizara ya Madini na taasisi zake kuongeza bidii na ufanisi katika kazi zao ili kuhakikisha Sekta ya Madini inafanikisha lengo la kuchangia asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.

Akizungumza Februari 8, 2025, katika Bonanza la Madini lililofanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari John Merlin jijini Dodoma.

Dkt. Kiruswa amesema kuwa ni muda wa kuongeza kasi ili kufikia na hata kuvuka lengo hilo muhimu kwa maendeleo ya taifa na kusisitiza kuwa juhudi za pamoja, uwajibikaji na mshikamano ndio msingi wa kufanikisha azma hiyo.

“Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2025 pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 vinaelekeza Sekta ya Madini kuchangia asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025. Tupo kwenye hatua za mwisho kufikia lengo hili, hivyo ni wajibu wetu kama watendaji kuhakikisha tunafanya kazi kwa weledi, bidii na mshikamano ili kutimiza azma hiyo,” amesema Dkt. Kiruswa.

Ameongeza kuwa, Sekta ya Madini imeendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa taifa, ikichangia ajira, Mapato ya Serikali, na maendeleo ya jamii kupitia miradi mbalimbali ikiwemo ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR).

Aidha, Dkt. Kiruswa amewataka watumishi wa Wizara ya Madini kuwa mfano wa utumishi bora unaojikita katika uadilifu, uwajibikaji na kuheshimu taratibu za kiutumishi na kuwahimiza kuhakikisha kuwa kila mtumishi anafanya kazi kwa juhudi na ubunifu ili kuboresha sekta hiyo.

“Wizara yetu ni kiungo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa taifa, hivyo kila mtumishi anapaswa kujitambua na kufanya kazi kwa bidii, uaminifu na ushirikiano. Tunapaswa kuwa mfano wa utumishi uliotukuka, wenye nidhamu na tija kwa manufaa ya nchi yetu,” ameeleza Dkt. Kiruswa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Mhandisi Yahya Samamba amewakumbusha watumishi wa Wizara na taasisi zake kuhusu wajibu wao wa kuhifadhi Siri Serikali na kuhakikisha kuwa taarifa nyeti zinahifadhiwa kwa mujibu wa taratibu za kiutumishi na kueleza kuwa ulinzi wa taarifa za Serikali ni suala nyeti linalohitaji umakini mkubwa, hasa katika sekta nyeti kama madini.

“Tunapotekeleza majukumu yetu, ni muhimu kuheshimu na kutunza siri za Serikali ili kulinda maslahi ya taifa. Utovu wa nidhamu katika suala hili unaweza kuathiri maendeleo ya sekta na kuleta athari kubwa kwa nchi,” amesisitiza Samamba.

Pia, Mhandisi Samamba amewahimiza watumishi wa Wizara na taasisi zake kuishi kwa upendo, mshikamano na heshima kati ya watumishi ndani na nje ya ofisi, akisema kuwa mshikamano ni silaha muhimu ya mafanikio. Aliwataka watumishi kufanya kazi kwa kushirikiana, kuheshimiana, na kusaidiana katika kutimiza majukumu yao ya kila siku.

“Tunahitaji kuwa na moyo wa kuheshimiana na kusaidiana. Umoja wetu ndio utakaotufanikisha kufikia malengo makubwa tuliyojiwekea. Kila mmoja awe sehemu ya suluhisho, si sehemu ya tatizo,” ameongeza Samamba.

Katika bonanza hilo, watumishi wa Wizara ya Madini na taasisi zake wametumia fursa hiyo kuwaaga rasmi aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof. Idris Kikula, na Kamishna Mstaafu, Prof. Abdukarim Mruma, ambao wamestaafu.

Mwenyekiti wa sasa wa Tume ya Madini, Bi. Janet Lekashingo, amewapongeza viongozi hao kwa mchango wao mkubwa katika kuboresha sekta ya madini na kuhakikisha sekta hiyo inazidi kukua na kuchangia katika kukuza uchumi wa taifa.

“Viongozi hawa wamefanya kazi kubwa na kwa weledi mkubwa. Watabaki kuwa kielelezo cha utumishi bora unaopaswa kuigwa na kila mmoja wetu. Tuna wajibu wa kuendeleza kazi nzuri waliyofanya,” amesema Bi. Lekashingo.

Bonanza hilo lilmehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Madini, taasisi zake ambazo ni Tume ya Madini, Shirika la Taifa la Madini (STAMICO), Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) pamoja Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI), lengo likiwa ni kujenga mshikamano miongoni mwa watumishi na kuhamasisha ari ya kazi kuelekea kufanikisha malengo ya sekta.








Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages