Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi ametoa wito kwa taasisi zote za kisheria na wadau wa haki nchini kutumia mifumo ya kidijitali kupata takwimu sahihi zitakazowawezesha kufuatilia migogoro yote waliyoisikiliza ili kuhakikisha inamalizika kwa mafanikio.
Dkt. Possi ametoa wito huo leo tarehe 01 Februari, 2025 alipotembelea mabanda ya maonesho ya taasisi mbali mbali nchini zinazoshiriki Maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini yanayoendelea kwenye viwanja vya Nyerere Square vilivyopo jijini Dodoma.
Dkt. Possi ameeleza kuwa matumizi ya mifumo ya kisasa yatasaidia kuboresha usimamizi wa haki na kuongeza uwajibikaji katika utatuzi wa migogoro ya kisheria kwa kuwa kwa kiasi kikubwa itawezesha kutoa takwimu sahihi na kwa haraka pale taasisi husika itakapohitaji kufahamu mwenendo wa mgogoro husika ulioshughulikiwa.
Akizungumza na watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Possi amesisitiza kuwa mifumo ya kidijitali ina uwezo mkubwa wa kuboresha utendaji kazi wa taasisi za kisheria kwa kuwezesha upatikanaji wa taarifa kwa wakati hatua itakayosaidia kuhakikisha migogoro yote inayoshughulikiwa kwenye kliniki za sheria inamalizika ili wananchi waweze kufanya shughuli zao za kukuza uchumi kwa amani.
“Kwa kutumia mifumo ya kisasa, tunaweza kufuatilia mwenendo wa migogoro yote kwa urahisi ili kuhakikisha migogoro yote inasimamiwa kwa weledi na kupunguza ucheleweshaji wa haki ili wananchi waendelee na shughuli zao za kujiletea maendeleo wao binafsi na taifa kwa ujumla,” alisema Dkt. Possi.
Alibainisha kuwa, matumizi sahihi ya mifumo hiyo yatasaidia kuondoa changamoto zinazoikabili Sekta ya Sheria nchini katika kushughulikia migogoro ikiwa ni pamoja na kupotea kwa nyaraka muhimu ambazo zimechangia ucheleweshaji wa maamuzi huku akisisitiza taasisi zinazohusika na usimamizi wa sheria kushirikiana katika kuunda na kutekeleza mifumo ya kidijitali inayolenga kuboresha uwajibikaji na uwazi.
Dkt. Possi alieleza kuwa mifumo hii itaiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi kuhusu migogoro inayoshughulikiwa, muda wa utatuzi wa migogoro husika na kiwango cha mafanikio ya migogoro inayosimamiwa na kumalizika kwa mafanikio makubwa hatua hii itatimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunajenga jamii imara isiyo na migogoro kwa kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani ili waweze kuendelea na shughuli zao za kujiletea maendeleo.
Akizungumzia namna Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inavyochangia kukuza pato la taifa, Dkt. Possi amesema kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imehakikisha wakati wote kuwa rasilimali za nchi zinalindwa ikiwemo miradi mikubwa ya maendeleo kama vile bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere, mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga, ujenzi wa madaraja makubwa ya Tanzanite na Kigongo Busisi Feri linalojengwa Jijini Mwanza ambayo miradi hii imekuwa chachu ya maendeleo katika kujenga na kukuza uchumi wa nchi.
“Miradi inalindwa kwa kuhakikisha kuwa utekelezaji wake hauathiriwi wala kukwama kutokana na migogoro na pale inapotokea changamoto Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inasimama kuhakikisha kuwa mradi hausimami, haukwami au kushindwa kutekelezwa kutokana na migogoro na Ofisi yetu imekuwa inashughulika kwa njia moja au nyingine katika uendelezaji wa miradi na kuhakikisha kuwa migogoro haiwi chanzo cha kuzuia utekelezaji wa miradi mbali mbali nchini”, amesisitiza Dkt. Possi.
Ameongeza kuwaOfisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imeendelea kuzishauri taasisi za Serikali ipasavyo pamoja na kumaliza mashauri nje ya Mahakama hatua ambayo imesaidia kupunguza migogoro na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Naye Afisa Mchunguzi Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria ndugu Laurent Bulilo amesema kuwa wamekuwa na kawaida ya kufuatilia migogoro na mashauri yote kupitia Mfumo wa Mama “8Samia Legal Aid Campaign System” hatua ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro kwenye jamii.
Djt. Possi ameonyesha jinsi Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inavyochangia kukuza pato la taifa kupitia usimamizi wa mali za umma, mikataba ya kimataifa na uimarishaji wa mazingira ya biashara.
Pia, ameahidi kuendelea kushirikiana na wadau wote wa sheria hasa wadau wa haki madai katika matumizi ya TEHAMA ili kuhakikisha mifumo inasomana ili kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa mashauri ya Serikali.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi, akiwasili kwenye viwanja vya Nyerere Square alipotembelea mabanda ya wadau mbalimbali wanaoshiriki Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea Jijini Dodoma kwa lengo la kuona namna wadau hao wanavyotekeleza majukumu yao.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi akizungumza na Mkurugenzi Msaidizi Usimamizi wa Mashauri wa Mahakama Kuu ya Tanzania alipotembelea Banda la Mahakama ya Tanzania kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea Jijini Dodoma.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi akimsikiliza Afisa Uchunguzi Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu Bi. Eugenia Lohay alipotembelea banda la Ofisi hiyo wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea Jijini Dodoma.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi akimsikiliza Afisa Uchunguzi Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Ndugu Laurent Bulilo alipotembelea banda la Wizara hiyo wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea Jijini Dodoma.
Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Ally Possi akisaini vitabu vya Taasisi zinazoshiriki Maadhimisho ya Wiki ya Sheria baada ya kutembelea mabanda ya maonesho ya Taasisi hizo kwa lengo la kuona namna Taasisi hizo zinavyotekeleza majukumu yao.
Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Ally Possi akiwa na watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwenye banda la Ofisi hiyo alipotembelea Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea Jijijni Dodoma.
Msajili wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Eva Nkya akimkabidhi cheti cha ushiriki wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria, Wakili wa Serikali wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, ndugu Salehe Manoro wakati wa maadhimisho hayo yanayoendelea Jijini Dodoma.