Imeelezwa lengo la Serikali la kuanzisha Vituo vya Mfano kwa ajili ya kutoa mafunzo ya uchimbaji bora kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini limefaniliwa kwa kiasi kikubwa baada ya wachimbaji wengi nchini kuhamia na kuanzisha teknolojia ya Uchenjuaji wa kutumia (CIP) badala ya mialo ambayo imesaidia kuongeza tija kwenye shughuli zao na kuondokana na uharibifu wa mazingira.
Hayo yamebanishwa na Mshauri Elekezi katika shughuli za uchimbaji mdogo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Tan Discovery Consultant Company Limited na mjenzi wa vituo hivyo, Mhandisi Rogers Sezinga wakati akizungumza katika mahojiano maalumu na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Madini baada ya kuvitembelea vituo hivyo.
Ameongeza kwamba, vituo vya mfano vimesaidia kuongeza mzunguko wa uuzaji madini kwenye masoko jambo ambalo limepelekea Serikali kupata taarifa za wachimbaji hao na hivyo kuwawezesha kupata mikopo kwenye baadhi ya taasisi za fedha hapa nchini.
‘’ Nikiwa mshauri elekezi, nimekuwa nikipata maombi mengi kwa ajili ya ujenzi wa CIP hizi kutoka maeneo mbalimbali nchini. Hadi sasa nimejenga CIP zaidi ya 10 na hapa kama mnavyoniona naendelea na ujenzi wa CIP nyingine, hivyo vituo hivi vimeongeza tija baada ya watu kujifunza. Wito wangu, wachimbaji wazitumie ili kuachana na matumizi ya zebaki na zitaongeza vipato vyao na kodi za Serikali,’’ amesema Sezinga.
Mbali na kuanzishwa CIP, vituo hivyo vimewavuta wakazi wanaozunguka vituo hivyo na wachimbaji kujikita kwenye shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya dhahabu baada ya kutoa elimu kwa vitendo kuhusu namna bora ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini kwa wachimbaji wadogo.
Vituo vya mfano vilijengwa na Serikali kupitia Wizara ya Madini katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo kilichopo kijiji cha Katente Wilayani Bukombe, Lwamgasa- Geita na Itumbi-Chunya, vinasimamiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) likisimama kama mlezi wa wachimbaji wadogo.
Aidha, mbali na mafunzo ya uchimbaji na uchenjuaji, vituo hivyo vinatoa huduma za uuzaji wa vilipuzi, kemikali, uchomaji wa kaboni ambapo mpaka sasa Vituo hivyo vimekusanya zaidi ya bilioni 3.3 zikitokana na kodi mbalimbali na mrabaha tangu kuanzishwa kwake Mwaka wa Fedha 2019- 2020.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Kituo cha Mfano cha Katente ambaye pia ni Mratibu wa Vituo vya Mfano vya Katente-Bukombe, Lwamgasa-Geita na Itumbi-Chunya, Mhandisi Tiberio Lucian Kaduma amesema Serikali kupitia STAMICO imejenga Vituo hivyo katika maeneo yenye madini kwa lengo la kumsaidia mchimbaji mdogo kupata maarifa ya uchimbaji na uchenjuaji bora na wenye tija.
Aidha, Mhandisi Kaduma amesema Vituo vya Mfano ni sehemu mahususi ya kuwapatia wachimbaji wadogo mafunzo ya nadhari na vitendo ili kukuza ujuzi, maarifa na elimu kuhusu uchimbaji salama na utunzaji wa mazingira.
Mhandisi Kaduma amesema Vituo hivyo vimesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza uelewa kuhusu uchimbaji salama ikiwemo uchenjuaji wa kutumia teknolojia ya sayanaidi katika uchenjuaji na kuachana na matumizi ya zebaki inayo haribu mazingira.
‘’Serikali kupitia STAMICO inampango wa kujenga vituo vya mfano vingine katika mikoa ya Kimadini ya Tanga Lindi na Kahama ili kuwasaidia wachimbaji wadogo kufanya shughuli za uzalishaji madini kwa faida na kuongeza tija kwenye Pato la Taifa.
Pamoja na mambo mengine, Mhandisi Kaduma ametoa wito kwa wachimbaji madini kote nchini kuvitumia Vituo vya Mfano kwa ajili ya maendeleo yao na kutumia huduma zinazotolewa na Vituo hivyo ikiwemo uuzaji wa vilipuzi na kemikali zinazotumika katika uchenjuaji madini ili kujiongezea wigo na ufanisi katika shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini nchini.
Kwa upande wake, mchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu wa Katente namba 1, Max Thomas Kajoro ambaye ni mnufaika wa kituo hicho, ameishukuru Serikali kupitia STAMICO kwa kujenga Kituo cha Mfano cha Katente ambacho kimemnufaisha kwa kiwango kikubwa baada ya kupeleka mawe yake kwa ajili ya kuchakata na kupata dhahabu nyingi zaidi ya matarajio yake ambapo ametoa wito kwa wachimbaji wengine kutumia Kituo hicho kwa ajili ya maendeleo yao.
‘’Kituo cha mfano Katente ni suluhisho na msaada mkubwa kwa wachimbaji wadogo ambapo mimi binafsi kimenisaidia kununua mashamba, gari, pikipiki, kujenga nyumba, kusomesha watoto na kukidhi kuhudumia familia yangu,’’ amesema Kajoro.
Naye, Mchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu wa Katente namba 2, Simon Sospeter Dittu ameipongeza Serikali kwa kujenga Kituo hicho katika eneo hilo ambapo amenufaika kwa kupata elimu ya uchimbaji salama na ushauri wa uchimbaji bora ikiwemo kutunza mazingira na elimu ya utambuzi wa maeneo yenye tija katika uchimbaji wa madini ambapo kwa sasa anazalisha kwa faida kupitia mgodi wake.
Kwa upande wake, Mchimbaji mdogo Pamela James amelipongeza Shirika la STAMICO kwa kuwalea vyema na kuwapa mafunzo ya uchimbaji na uchenjuaji kwa vitendo jambo ambalo limewasaidia wachimbaji wengi kuachana na mila potofu za kutumia waganga na badala yake kutumia utaalamu waliyopatiwa na kujipatia faida ambapo kwa sasa mama huyo ameajiri zaidi ya wafanyakazi 50 katika shughuli zake za uchimbaji.
Aidha, Pamela ametoa wito kwa STAMICO kupanua wigo wa uzalishaji kwa kufunga mitambo mikubwa zaidi ili kupunguza foleni ya wateja, muda na kuongeza uzalishaji tofauti ya ilivyo sasa.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEi8Bcz2ws8ijQxcZkN4QJgyt6Dp9ASRfn5do1f7fuv8NLbz721xCSfTUlr-ME2MDL5ItLP9fe8xPHf9ba2QJk2CorRObXCqBWmFGP8lDqbzv6xNOumDMM6q4vzkztcw0eZIVUp_E7zldfX6uZz48HL4mFgtoJYyJjrdPTSrVz0CPGyKR_-MA_em_LfOgmuT/s1600/IMG-20250209-WA0033.jpg)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjdk2hCGkfc2HvnmLR61Wi5L1bpwzP-Fn19gjgmiHJZ5mUacvBIol_NzVIMylO6SeOEKkMvfTcTOffr2p4DQWY0nPdHfvfDGo4ur2F3mrICgAhVZCHba80M22f1tsURD-uAF1Ig3zweLOHlqcGFWfaoESBrQLV04NScgnwaSRtwn-Dnuwwz4wJfMXHl5sgy/s1600/IMG-20250209-WA0032.jpg)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEh99DTpnvPnj6rq98tBU3KGtz0OKjEpmgJyAaq45mDON5U0jg5-te8-PwLUKX9WiNpZcG3kUFFRWDbzTNOfD2x7J8oPYAA64VK5EjNjKePBD2yifRHWFE6W0DvQzN0wZeWe1JHO9Ts5U4uUEb72-UiCNLLIM2hS7rg0zlovZm7I6YGSJooW4GqPCDdzaAv9/s1600/IMG-20250209-WA0031.jpg)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhSDm1TIqDgGuYkRzjGQnhvrfk1FX__tD2F507f3tbegX3PmucCj3i4y9-LlEGfQnD5l4yAIvFAXiIksfcEL8Csz6ZFbWKRaUCnC8RLpjwYV7fNl7ubGCJxmDcwkJDy6UQUcpDLqdrEomzwrCLbnonB8DdboGmKmhsRlgujl5-etXOtOgSank3Nk_CH-umj/s1600/IMG-20250209-WA0030.jpg)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgWJPr8JljJsEmJrX1BQI_qQIvLxXSWe36J5y17yYREM0qDwu6I_HUp8h8BhSUZVbE1H5kElUdpOjZUL_PznCVEYGRcVUG9C8VT68ENwqDO2WXG57rDoFllOFfDn-rIWO7RkVnJIPTeUYmLsA8WhjhqqahPn-nzSE_RRK1W30vQ5HXo4mjsorCs7MTijhys/s1600/IMG-20250209-WA0041.jpg)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEj37JG9jWuMkkZ_dgn22wezCadDN7QiIVfOD195twj4sy6KSMi4xmtXXkvO56AmmBMovCSz2Ks6Sdp1Iucl85ZTDB80WTpFzBWEyNVRp8bxAbZPrXZalvn4x_3K-1wagdICmKnY2VUZlybRRgwkSxJiQ6uW2HC6maztIErAeRm_OcYU81Ew3hgE3PHEHSi1/s1600/IMG-20250209-WA0029.jpg)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgF0lM2eGvC1A3j4Xn0FQ4fRP_GZT5ko9vhNr1bHNwJmsezKiobsUyHM2gH44IIdTH_RElxgcwoFM9XFDc0D1T0J3yIKjnu346sJFTz-Y8VX-1VZoZpSWDK44N0OJWl_a4RLkiNkjayiRKKDLtX6WxhJIwHqW7lI47H_MBYAv1ZeZ30I3Wme1kfu5tm4Enq/s1600/IMG-20250209-WA0040.jpg)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgoTZjgzt51TVLAPiQR2tnXzyPeJGU8aKjp2L0eT8wZArH0TAwCmERrclasRnEkroYyV8neWihIrUA7epC4TSmpXMKwMH9uMIS91JygJzw_0mAX_vRNFs1Nq6syJoFsp2uSz9pCdu_R6eIg8JEwG4TA0KNXAn5FlwkGNskooXz3Eczpn8DGJDwBZjMwT2c8/s1600/IMG-20250209-WA0039.jpg)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgk4znGObgnEzJwAvE9gA8NiDfFVuQkklb9IZ_O3IPsPVy9OllTH5rkhAK-zKwIcD75yNueJOgFnmILFnXebB7botMGqLfglRoyVONN9_J4P7zHpyPPh80DT9duvbo5ce3_FYGAEpM56ITkFuPRrgCVLeB1_NQVBN8PXL80tvZ5lDWNcLXvpiD8ReVhQSV5/s1600/IMG-20250209-WA0038.jpg)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgvIQe_zdCHIht3btElSNDCDSS2dwDRXT7HGAQXbuz57j8BKgnE3ke-LQHsUM8IiMD5I940b_l5JeUndSdrv0ou6FvOz-z3GV4j3byumCB2VZCt_SVo03ItsKIBnQ2drU4s9BpYFlqM3jB4LYl6zKh38MIVHToVLpksnA9x431y-svGci_EjGZ2WJeVFQZ0/s1600/IMG-20250209-WA0037.jpg)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgat3rPYsPidmJxrB8HZyP3mcx2x09oAvPcSshJDbI2zPfK3r4BgzKa63i5YrTrhChwMWFm9tXfFmRlAaVF4Kmcz_sXlmxT0_alXGXISax86f0snQflxUwYHtCQHHChkqO9p0aiE7uY0l5lINoIzv9dkTF8ZIjFrtCMCna64CWur7JVC0yKMyznzjlGE4Q2/s1600/IMG-20250209-WA0036.jpg)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjDJW_RXNQCEE6O9hLiIwWwByz7ruZq_ZwWjwW0B3vqBe836PdrSz9mgGhP7NDqpKW4SGq2XQknfUEfRK2Rhrj7cELvqABQ9HZG9r2BTLYr1-vwuQ1DzLAfdtl4F28n98GGuuaoxsUxaz7EOwfygSbzNNEkji6ojRxB5fjxW-sorWhD38I5YYG7ZNy4wyss/s1600/IMG-20250209-WA0035.jpg)
*xxxxx xxxxxx xxxx*