NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
SERIKALI ya Mtaa wa Muungano Marobo kata ya Goba Wilaya ya Ubungo, Jijini Dar es salaam imepiga hatua kubwa ndani ya miezi miwili ya uongozi mpya ulichaguliwa Novemba 27,2024 katika sekta ya maji,elimu pamoja na suala la uchumi ambapo katika upande wa sekta ya maji tayari wamefanikiwa kupeleka mabomba kwaajili ya kuwaunganishia majisafi wananchi wao.
Hayo yameelezwa leo Februari 9,2025 Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Mtaa huo, Isack Maduhu wakati wa kikao na wananchi wake kwa lengo la kutoa taarifa ya utendaji kazi.
Amesema katika utekelezaji wa miradi hiyo tayari wamepeleka mabomba katika Shina namba nne, na shina namba tano na wananchi tayari wameshaanza kuchukua fomu kwaajili ya kuunganishiwa na huduma hiyo.
"Shina namba tatu na shina namba moja tayari yamepatiwa mabomba kwa ajili ya kuunganisha huduma ya maji safi". Amesema
Vilevile, Maduhu ameeleza kuhusiana na suala la uchumi ambapo wameamua kuanzisha mnada katika eneo la Malogo Senta ambao utakuwa ukifanyika kila siku ya ijumaa.
Katika upande wa sekta ya Elimu, Maduhu amesema serikali yao ya Mtaa imefanya ziara katika eneo la shule ya msingi ili kujua Mazingira halisi ya watoto wanapopatia Elimu ambapo walikutana na kamati ya shule nakushauriana kuandika barua kwa ajili ya kuongeza vyumba vya madarasa kwa ajili ya watoto wa awali sambamba na matundu ya vyoo.
Sambamba na hayo, Maduhu amesema kuwa katika upande wa ulinzi na usalama wamejidhatiti kuhakikisha wajumbe wanajua watu wao ili kupunguza vitendo vya uhalifu.
Kwa upande wake,Mwakilishi wa TARURA Mhandisi Cavine Lugendo ameeleza changamoto inayokwamisha ujenzi wa Barabara ya Makonda pamoja na za Mtaa wa Muungano ni ukosefu wa fedha kutoka serikali kuu.