Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imewahakikishia wananchi waliopisha Ujenzi wa Barabara ya Ntyuka -Mvumi- Kikombo (Km 76) kulipwa fidia ya kiasi cha Shilingi Bilioni 7.4 mara baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria.
Akizungumza jijini Dodoma, Februari 9, 2025 Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema mpaka sasa Serikali imeshalipa kiasi cha Shilingi Bilioni 20 kama fidia kwa wananchi waliopisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Barabara nchini hivyo utekelezaji wa mradi huo pia utaenda sambamba na malipo ya fidia kwa wananchi hao.
“Niwatoe hofu katika hili, niwahakikishie kuwa mara baada ya mchakato wa kisheria kukamilika kila mwananchi atalipwa anachostahili”, amesema Ulega.
Aidha, Waziri Ulega amewaagiza wakandarasi CHICO na China First wanaotekeleza mradi huo kurudi katika eneo la mradi na kuendelea na kazi ya ujenzi wa barabara hiyo kwani Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza miradi hiyo kutekelezwa na tayari Serikali inaendelea kutoa fedha ili iweze kutekelezwa na kukamilika kwa wakati.
Ulega ameongeza kuwa Rais Samia anaendelea kulifungua jiji la Dodoma kupitia miundombinu ya Barabara ambapo amesema kuwa miradi mbalimbali ya barabara inatekelezwa na mingine inatarajiwa kutekelezwa ikiwemo ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma na mpango wa kujenga barabara ya njia Sita kutoka Chamwino Ikulu kuingia katikati ya jiji.
Kadhalika, Waziri Ulega ameuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanaziba mashimo yaliyopo katika Barabara inayopita mtaa wa Abdu Jumbe na Mvumi eneo la Kilimani jijini Dodoma kwani yamekuwa kero kwa wananchi wanaotumia barabara hizo pamoja na kufunga taa ili barabara iweze kupendeza na kuwa na nuru wakati wa usiku.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini na Mbunge wa Dodoma Mjini, Antony Mavunde amesema kuwa barabara ya Ntyuka - Mvumi- Kikombo ni barabara ya kihistoria hivyo ameomba Serikali kukamilisha barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwani ni mkombozi kutokana na uwepo wa hospitali kubwa ya macho ya MVUMI inayotoa huduma nchi nzima na pia kuunganisha maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Dodoma, amaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa ujenzi wa barabara hiyo kwani mradi huo tayari umenufaisha wananchi 201 kwa kutoa ajira za muda hadi sasa.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi, Mohamed Besta amesema kuwa
Ujenzi wa barabara ya Ntyuka - Mvumi- Kikombo unatekelezwa kwa Sehemu mbili ambapo sehemu ya kwanza kutoka Ntyuka- Mvumi- Makulu na Kikombo - Chololo -Mapinduzi (Km 25) inatekelezwa na Mkandarasi CHICO kwa gharama ya shilingi Bilioni 38.1 na sehemu ya Pili ya Ntyuka -Mvumi Hospitali - Kikombo (Km 53) inatekelezwa na Mkandarasi China First kwa gharama ya Shilingi Bilioni 98.4.