Breaking

Saturday, 1 February 2025

NCHIMBI: CCM NA PP KUIMARISHA UHUSIANO WA TANZANIA NA ETHIOPIA


KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amesema urafiki kati ya CCM na Prosperity Party, chama tawala cha Ethiopia, ni hatua muhimu katika kuboresha na kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili, pamoja na watu wake.

Balozi Nchimbi amesema kuwa ushirikiano mzuri kati ya Tanzania na Ethiopia umebebwa kwenye misingi imara ya itikadi za kisiasa iliyowekwa na waasisi wa nchi hizo mbili, akitoa wito kuwa uongozi wa kizazi cha sasa unawajibika kuimarisha zaidi kwa ajili ya manufaa ya kiuchumi ya wananchi wa pande zote.

Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Nchimbi amesema hayo alipokuwa akitoa salaam za CCM kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha PP, uliofanyika mjini Addis Ababa, tarehe 31 Januari 2025, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi nchini Ethiopia.

“Kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunawapongeza sana wenzetu wa Prosperity Party, chini ya uongozi wa Rais wa Chama, ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Abiy Ahmed.

“Uongozi wake madhubuti umekuwa mojawapo ya chachu na nguzo imara kwa maendeleo makubwa ambayo Ethiopia imepiga hatua kubwa kwa miaka ya karibuni, katika nyanja mbalimbali za kiuchumi,” amesema Balozi Dkt. Nchimbi.

Balozi Nchimbi ameongeza kusema kuwa kupitia urafiki wa vyama hivyo viwili, ushirikiano wa Serikali, nchi na hatimae uhusiano baina ya watu wa pande hizo mbili utakuwa wa kupigiwa mfano, kwa ajili ya watu wote wapenda maendeleo ya watu na vitu kwa ajili ya ustawi wa jamii nzima.

“Tunapenda kukuhakikishia Mhe. Abiy kuwa Tanzania na Serikali yake, inayoongozwa na CCM chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tutaendelea kushirikiana na PP, Serikali ya Ethiopia, kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi ya watu wa nchi zetu mbili ambao wametupatia dhamana ya kuwatumikia,” amesema Balozi Dkt. Nchimbi.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages