WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umepokea wawekezaji kutoka Kampuni ya FIT Group kutoka nchini Nigeria. Ujio wao ni wa mara ya pili ambapo wawekezaji hao wamekuja kuona maeneo ya uwekezaji yanayomilikiwa na TBA kwa ajili ya kuyaendeleza kwa njia ya ubia. Ziara yao nchini imeambatana na kufanyika kwa kikao kati yao na TBA pamoja na kutembelea maeneo ya uwekezaji.
Katika Kikao hicho wawekezaji hao kutoka FIT Group walipokea wasilisho la mpango wa uendelezaji na kuonyeshwa fursa za uwekezaji zilizopo kwenye meneo hayo pamoja na kuyatembelea.
Akizungumza baada ya kutembelea maeneo ya Magomeni Kota, Kindondoni Manyanya Kota pamoja na Ilala Mchikichini Kota jijini Dar es Salaam, Mshauri Elekezi wa Kampuni hiyo Bw. Godbless Safugha amesema kuwa kikao na ziara hiyo imetoa nafasi ya kuona Mpango wa Uendelezaji wa maeneo pamoja na miradi inayotekelezwa na TBA.
“Tunatarajia kufanya uwekezaji katika nchi za Afrika Mashariki, lakini tumevutiwa zaidi na Tanzania hasa maeneo mazuri ya TBA katika jiji la Dar es Salaam na Dodoma ambayo yanatoa fursa ya uwekezaji hasa katika Sekta ya majengo”.
Pia Bw. Godbless amesema kuwa uwekezaji huo unatarajia kugharimu kati ya dola za marekeni milioni 30 mpaka 40 na kutoa ajira zaidi 10,000 kwa vijana wa Kitanzania.
Vile vile Bw. Godbless amesema kuwa wanatarajia kusaini Hati ya Ushirikiano (MoU) kati ya Kampuni yao ya FIT Group na TBA ndani ya muda mfupi ujao kabla ya kusainiwa kwa mikataba ya uendelezaji.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Miliki Bw. Fredy Mangula amesema kuwa ziara ya Kampuni ya FIT Group imekuwa na tija na kuwa TBA inaendelea kuwakaribisha wawekezaji wengine wa ndani na nje ya nchi kutembelea maeneo ya uendelezaji yaliyopo katika mikoa yote nchini ili waone fursa za uwekezaji zilizopo kutokana na changamoto ya upungufu wa nyumba bora za makazi katika mikoa hiyo.
Vile vile Bw. Mangula amesema kuwa kuja kwa wawekezaji hao ni matokeo ya utekelezaji wa agizo lililotolewa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Machi 21, 2022 wakati wa ufunguzi wa nyumba za waakazi 644 katika eneo la Magomeni Kota jijini Dar es Salaam.