Breaking

Tuesday, 11 February 2025

EWURA YAWAPIGA TAFU VIJANA WAJASIRIAMALI SONGEA


Meneja wa EWURA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi. Karim Ally, akimkabidhi Tanki la Kuhifadhia maji na vifaa vyake, Mkuu wa Wilaya ya Songea Mjini, Mhe. Wilman Kapenjama, ili awakabidhi vijana wajasiliamali wa Wilaya hiyo, leo 11.2.2025. Songea.


Na.Mwandishi Wetu


Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imewapiga tafu vijana wajasiriamali wa Wilaya ya Songea mjini, Mkoa wa Ruvuma, wanaojihusisha na shughuli za kilimo cha kahawa na mbogamboga kwa kuwapatia vifaa vya umwagiliaji.

Akikabidhi vifaa hivyo, Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi. Karim Ally, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, alikabidhi, tanki moja la kuhifadhia maji, lenye ujazo wa lita 5,000, mpira na vifaa vya kuunganisha na kufunga tanki hilo ili vikawasaidie vijana hao, katika shughuli zao za kilimo.

Mhandisi. Ally alisema, EWURA ina jukumu la kuleta matokeo chanya katika kukuza na kuendeleza ustawi wa jamii kwa ujumla, na ili iweze kufikia lengo hilo, imetenga bajeti ya kuchangia na kutoa misaada kwa jamii kwa mujibu wa sera yake ya CSR.

“EWURA pia inajukumu la kusimamia utunzaji wa vyanzo vya maji , hivyo uwekaji wa miundombinu sahihi kwaajili ya umwagiliaji wa mazao yao utasaidia katika utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla” alisema Mha.Ally.

Akipokea vifaa hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Songea Mjini, Mhe. Wilman Ndile, aliwashukuru EWURA kwa kuwapatia vifaa hivyo kwani itawaepusha vijana hao kuharibu mazingira kwa kuchimba mifereji kienyeji na kwamba miundombinu hiyo itawasaidia kufikia lengo la wilaya hiyo kuwa na miche milioni moja ya kahawa kwa wakulima wadogo wadogo.

Kwa upande wake Katibu wa kikundi hicho, Bw. Benedict Mbawala aliwashukuru EWURA kwa kuwasaidia lakini pia Mkuu wa Wilaya kwa kuwasiliana na EWURA ili wapate vifaa hivo.




Meneja wa EWURA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi. Karim Ally, akimkabidhi Tanki la Kuhifadhia maji na vifaa vyake, Mkuu wa Wilaya ya Songea Mjini, Mhe. Wilman Kapenjama, ili awakabidhi vijana wajasiliamali wa Wilaya hiyo, leo 11.2.2025. Songea.

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Wilman Kapenjama, akimkabidhi tanki la kuhifadhia maji kwaajili ya kilimo cha kahawa na mbogamboga, Katibu wa Kikundi cha Vijana Wajasiriamali wa Songea, Bw. Benedict Mbawala, leo 11.2.2025
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages