Katibu
Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mgombea Mwenza wa Urais Tanzania
Bara, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewahimiza wanachama wa Jumuiya ya
Umoja wa Wazazi kuendelea kujipanga vyema ili kuhakikisha chama
kinashinda kwa kuzingatia sera na maadili.
Akizungumza
wakati akipokelewa kabla ya kikao cha Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya
hiyo jijini Dodoma, Dkt. Nchimbi alisisitiza kuwa CCM ni chama
kinachojikita katika sera na maendeleo, si katika matusi au kejeli.
"Chama
chetu kimefanya mambo makubwa kwa maendeleo ya taifa. Tunapaswa
kuendelea kusimamia hoja zenye mashiko na si kutumia lugha zisizofaa.
Tunapaswa kuwa mfano wa kuheshimu watu na kuzungumzia maendeleo
yanayoonekana," alisema.
Aidha, alieleza kuwa serikali
inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanikisha mambo mengi
ambayo yanaweza kuwahamasisha wananchi kuendelea kukiamini chama.
"Tunayo
mengi ya kuwaambia Watanzania kuhusu maendeleo yaliyofikiwa, hatuna
sababu ya kutumia lugha za kejeli. Hayo tuwaachie wale wasiokuwa na hoja
za msingi," aliongeza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Umoja wa Wazazi Taifa, Fadhili Maganya, alisema kuwa ujio wa Dkt.
Nchimbi katika kikao hicho ni ishara ya heshima kwao.
"Uwepo wako
hapa umetupa faraja kubwa. Tumekukaribisha ili usikilize mawazo yetu na
kutushauri. Hii ni historia, kwani sisi ndiyo jumuiya ya kwanza kuketi
na wewe tangu uteuliwe kuwa mgombea mwenza," alisema Maganya.
Kikao
hicho kilitoa fursa kwa viongozi wa Umoja wa Wazazi kujadili masuala
muhimu yanayohusu ustawi wa jumuiya na mchango wake katika mustakabali
wa chama kuelekea uchaguzi ujao.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John
Nchimbi akizungumza kwenye Kikao cha Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu
la Umoja wa Wazazi, Jumuiya ya CCM, ambacho alialikwa na kushiriki
akiwa mgeni maalum, leo Jumamosi tarehe 8 Februari 2025, katika Ukumbi
wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.