Breaking

Friday, 7 February 2025

AZIMIO LA BEIJING: MIAKA 30 YA MAPAMBANO YA USAWA WA KIJINSIA



NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MWAKA 1995 Mkutano wa 4 wa kimatifa wa wanawake ulifanyika Beijing China na uliangazia masuala mbalimbali ambapo washiriki kutoka nchi maskini na tajiri walipitisha mwongozo wa utekelezaji wa Mkutano wao kwa miongo miwili iliyofuata.

Mwongozo huo ulibeba kurasa 129 na vipengele 12 vya kuzingatia,ambapo miongoni mwa masuala yaliyopitishwa kushughulikiwa ni umaskini, elimu na mafunzo, afya, mizozo ya kivita, uchumi, Mfumo wa Uongozi na upitishaji maamuzi, mifumo ya kitaasisi, haki za binadamu, vyombo vya habari, mazingira na mtoto wa kike ambapo Katibu Mkuu wa mkutano huo wa Beijing wa wakati ule alikuwa ni Bi.Getrude Mongela.

Licha ya maazimio hayo ya haki msingi za wanawake zilizovaliwa njuga miaka 30 iliyopita bado zinaendelea kudorora na usawa wa kijinsia kubakia katika hali Tete ambayo bado inaonesha kuna safari ndefu kufika katika hatua nzuri.

Akizungumza katika Kongamano la wanawake Viongozi walipokuwa wakisherehekea miaka 30 ya Beijing Disemba 2024 Jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) Bi.Lilian Liundi alinukuliwa akisema wanawake asilimia 2.1 pekee ndio walijitokeza Katika kuwania nafasi za uongozi wa vijiji na serikali za mitaa katika uchaguzi ulifanyika mwaka huo jambo ambalo linaonesha kasi ndogo ya ushiriki wa wanawake katika masuala ya Uongozi.

Sambamba na hayo,Katika miaka ya karibuni wanawake wameibuka katika sekta mbalimbali, iwe ni katika masuala ya siasa, uongozi, biashara, sayansi na teknolojia, na hata zile kazi ama sekta ambazo zilikuwa zinatawaliwa na wanaume, wanawake kwa sasa nao wamejitokeza na kuwa sawa au hata kuwazidi wanaume.

Katika mahojiano yaliyofanyika Oktoba 01,2020 na kituo Cha habari Cha umoja wa Mataifa UNIC na aliyekuwa katibu mkuu wa Mkutano huo Bi.Getrude Mongela alipoulizwa baada ya 25 hali iko vipi alisema.

“Miaka 25 sasa imepita tumeangalia yote tuliyokubaliana Beijing, tumeona tumepiga hatua kiasi gani. Inapokuja kwenye suala kama elimu, mataifa mengi yamekubaliana kutekeleza usawa kati ya mtoto wa kike na wa kiume. Na Tanzania nadhani tumefanya kazi nzuri zaidi, na jambo ambalo limenifurahisha zaidi rais wetu na serikali yake ya awamu ya 5, amechukua uamuzi wa kuhakikisha watoto wote wa shule hawalipi karo tangu wanapoanza shule hadi anapomaliza kidato cha 4. Watu wengi labda hawajui, hayo ni mapinduzi makubwa. Tuliposoma sisi, tatizo lilikuwa moja asomeshwe mtoto wa kike au wa kiume.”

Aidha Bi.Mongela alisema katika kipindi chao walikuwa na matatizo mengi walipoenda Beijing walibaini mwanamke kukandamizwa Hadi kwenye mshahara ambapo mwanaume alivyolipwa haikua sawa na mwanaume jambo ambalo sisawa.

"Ilikuwa malipo ya mwanamke wanafanya kazi ile ile, ni mwalimu kama mwalimu wa kiume lakini mwalimu wa kiume atalipwa zaidi kuliko mwalimu wa kike, au daktari wa kiume atalipwa zaidi kuliko daktari wa kike. Hayo nayo yamesawazishwa. Tumekuwa na hatua mbalimbali kila sehemu lakini bado tuna changamoto"Alisema

Katika hatua nyingine Tanzania kama moja ya nchi zinazoendelea katika ukanda wa Afrika,imepiga hatua kubwa katika sekta ya afya ambapo kupitia serikali ya awamu ya sita imejipambanua kuhakikisha kunakuwa na huduma ya afya Kila Kata kwa lengo la kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Hata hivyo Afisa Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) Idara ya ujenzi wa nguvu za pamoja Flora Ndaba kwenye Mafunzo ya Vijana na Mashirika mbalimbali Disemba 29, 2024 alisemaTanzania imepiga hatua kubwa katika kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia mikakati mbalimbali kama asilimia 10 ya mapato ya halmashauri, mifuko ya uwezeshaji wanawake kiuchumi, na majukwaa ya uwezeshaji.

Pamoja na hayo,mashirika yasiyo ya kiserikali nchini yalieleza kuwa serikali imepiga hatua katika kutokomeza ukatili wa kijinsia,ambapo vitendo vya ubakaji,ukeketaji na ukatili wa kijinsia kwa ujumla vimepungua ingawa juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha changamoto hizo zinatokomezwa.

Azimio la Beijing, linalotarajiwa kuadhimishwa Mapema Machi 2025 jijini New York, Marekani ambapo watangaazia Mambo mbalimbali waliyoyafikia katika azimio lao la Beijing katika miaka 30 iliyopita

Mkutano wa kwanza wa kimataifa wa wanawake ulifanyika Mexico City nchini Mexico mwaka 1975, na wa pili ulifanyika Copenhagen, Denmark mwaka 1980 na kisha Nairobi Kenya mwaka 1985 na miaka 20 baadaye Beijing China mwaka 1995.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages