Breaking

Tuesday, 28 January 2025

WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YABORESHA UTAWALA BORA KIGOMA


Viongozi wa Halmashauri ya Kigoma wameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuanzisha mafunzo kwa maafisa wa wilaya hiyo kuhusu utawala bora na sheria.

Wakizungumza baada ya kupata mafunzo hayo, baadhi ya washiriki wamesema kuwa ubunifu uliofanywa na Wizara ya Katiba na Sheria utasaidia kuboresha utendaji kazi wa watumishi na kufuata misingi ya utumishi bora na sheria.

Bwana Charles Fredy, ambaye ni mshiriki wa mafunzo hayo, amesema kuwa mada zilizotolewa na wakufunzi wa mafunzo hayo zinasaidia kuwakumbusha wao kama watumishi wa umma kufuata sheria na taratibu za kazi.

Naye Bi. Petronia Bwakila, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Taka na Mazingira kutoka Kigoma Mjini, amesema kuwa mafunzo hayo yanawakumbusha kutambua haki na wajibu wao katika kutekeleza majukumu yao pindi wanapowahudumia wananchi. Ameiomba serikali kuongeza muda zaidi wa mafunzo hayo ili kuwajengea uelewa zaidi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mjini, Bw. Rashid Chuachua, amempongeza Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damasi Ndumbaro, kwa kutoa mafunzo hayo ngazi za juu na kuwafikia wananchi wa ngazi za chini.

Amesema kuwa wizara hiyo imefanya jambo la msingi kwa kuwapatia viongozi hao mafunzo, huku akiwataka watumishi kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia maadili pamoja na sheria za kazi.







Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages