Breaking

Monday, 13 January 2025

Wasanii wa Kitanzania Kufaidika na Mirabaha ya Muziki Kupigwa Viwanja vya Ndege

Na Grace Semfuko, Maelezo

Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma na Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile, wameshuhudia utiaji saini makubaliano ya matumizi ya asilimia 80 ya muziki wa wasanii wa kitanzania, kupigwa katika viwanja vya ndege nchini, ili kuwawezesha kufaidi matunda ya kazi zao yatokanayo na malipo ya mirabaha.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa na Msimamizi wa Haki Miliki (COSOTA) Bi. Doreen Sinare, na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bw. Abdul Mombokaleo, ambapo Katika makubaliano hayo, imependekezwa muziki wa wasanii wa kitanzania kusikilizwa zaidi, lengo likiwa ni kulinda kazi za sanaa za watanzania pamoja na kuutangaza muziki huo ndani ya nchi na nje kwa wageni wanaoingia na kutoka nchini kila siku.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe.Mwinjuma amesema kusainiwa kwa mkataba huo ni nia ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha mazingira ya wasanii.

"Rais alionyesha nia ya kuboresha mazingira ya wasanii kwa kutambua mchango wa sanaa katika Taifa letu na umuhimu wa kazi zao, na pia kutafuta njia za ziada za kukuza kipato chao pamoja na uchumi, leo tumefikia hatua muhimu ambapo COSOTA imefikia Makubaliano ya Ushirikiano na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kuhusu suala la kulipia leseni (mirabaha) kwa matumizi ya muziki katika viwanja vya ndege. Makubaliano haya, ambayo ni sehemu ya Mkataba kati ya TAA na COSOTA, yatasaidia wasanii wa muziki wanapata haki yao ya malipo kutokana na matumizi ya muziki katika maeneo ya viwanja vya ndege nchini." Amesema Mhe. Mwinjuma.

Amesema hiyo ni hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa wasanii wanapata masoko ya kazi zao, na kupata mapato kutokana na vyanzo mbalimbali vya kazi zao, na kwamba haki zao zinaheshimiwa kikamilifu.

Aidha ameongeza kuwa katika kipindi cha Septemba 2023 hadi Novemba 2024, COSOTA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikusanya zaidi ya shilingi Bil. 1.1

"Itakua vema pia nikisema kuwa katika kipindi cha Septemba 2023 hadi Novemba 2024, COSOTA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya jumla ya shilingi bil. 1.1 ambazo zitagawanywa kwa wanufaika ambao ni Wasanii, Waandishi wa muziki, filamu, sanaa za maonesho, na sanaa za ufundi.

Nae Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile amesema taasisi za COSOTA na TAA zimekuwa za kwanza kuingia makubaliano ya namna hiyo na kutoa wito kwa taasisi zingine za usafirishaji zilizopo kwenye wizara yake, kuiga mfano huo ili kuwanufaisha wasanii kupitia kazi zao.

"Kwa taarifa nilizonazo katika taasisi zetu zote za wizara ya uchukuzi, TAA inakuwa ya kwanza kuingia makubaliano haya, natoa wito kwa taasisi zingine hususan Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), na Kampuni ya Meli Tanzania (TASHIKO) kuwasiliana na COSOTA na kuiga mfano mzuri uliowekwa na TAA" amesema Mhe. Kihenzile.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages