Breaking

Thursday, 30 January 2025

WANAHARAKATI WA JINSIA WAOMBA MAZINGIRA WEZESHI KUPANDISHA UFAULU WA MTOTO WA KIKE

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

WADAU wa semina za jinsia na maendeleo (GDSS) wameiomba Serikali kuongeza juhudi za kujenga mazingira wezeshi yatakayo msaidia  mtoto wa kike kufaulu kwa viwango vya juu kama ilivyo kwa vijana wa kiume.

Ombi hilo limetolewa Januari 29,2024 Mabibo-Jijijini Dar es Salaam katika semina za jinsia na Maendeleo (GDSS) zinazofanyika Kila wiki Jumatano,

Mwanaharakati wa Jinsia na Maendeleo Kennedy Anjelita akichangia maoni yake amesema kuwa changamoto  ya upatikanaji wa chakula shuleni ni moja ya sababu ambayo inapelekea watoto wa kike kutofaulu vizuri kwa kupata alama za juu.

Hata hivyo ameongeza kuwa wasichana wamekua wakiharibiwa kisaikolojia katika jamii kwenye makundi ya vijiweni wakiwemo bodaboda kwa kuwaingizia mabinti  habari za masuala ya mahusiano ya kimapenzi wakiwa shuleni jambo ambalo limekua likizorotesha  ufaulu kwa wanafunzi wa kike pale wanaposhawishika kuingia katika masuala ya mahusiano.

Aidha ameeleza kuwa suala la hedhi salama pia limekuwa kikwazo kikubwa kwenye ufaulu wa wasichana kwani mabinti wengi wamekuwa wakikosa vipindi kutokana na mazingira hafifu ya kujistiri wanapokua katika hali hiyo.

Pamoja na hayo, Anjelita ameshauri kuwa wazazi wanatakiwa kumpunguzia majukumu ya nyumbani mtoto wa kike kwa kufanya mgawanyo wa kazi  kwa vijana  wa kiume ambao wapo katika familia ilikumsaidia mtoto wakike  asichoke kupitiliza naye apate nafasi ya kujisomea.

"Wazazi wao wanaona kama wanamfundisha kazi binti yao kumbe wanamuharibu kisaikolojia wakati yeye anahtaji kusoma wao wanamlimbikizia kazi". Amesema Anjelita.

Vilevile,Anjelita  amesisitiza kuwa wazazi wanapaswa kutenga bajeti kwenye familia zao kwa ajili ya taulo za kike ili pale binti atakapokuwa katika siku za hedhi awe na uhakika wakuzipata.

Kwa upande wake mdau wa Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) Dolice Alchard amebainisha kuwa changamoto ambayo inachochea ufaulu hafifu kwa watoto wakike  ni pamoja na umbali mrefu kutoka sehemu anayoishi hadi shule inapopatikana ambapo msichana  hadi anapofika shuleni kutokana na mabadiriko ya ukuaji anakua tayari amechoka na hawezi kuelewa pale anapofundishwa.

Aidha Dolice ameendelea kwa kusema kuwa wazazi wameridhika na kuwaachia watoto wao walimu pekee,kwa ajili ya kuwafundisha ambapo  hawafatilii binti zao kile walichojifunza shuleni wala kuhtaji kufahamu Maendeleo yao.

Dolice ameeleza kuwa wasichana wengi wamekuwa wakikosa elimu ya kujitambua kuanzia  nyumbani kwao wakiwa wadogo jambo ambalo limewafanya kunasa katika mtego wa vishawishi wakiwa na umri mdogo kwani anakua haelewi  masuala ya uzazi hadi anapofikia katika umri wa kujitambua tayari anakua ameharibikiwa.

Pamoja na hayo,Dolice amesisitiza kuboreshwa kwa miundombinu ya usafiri pamoja na mazingira wezeshi yatakayomsaidia mtoto wakike  kujistiri anapokuwa kwenye hedhi pamoja na kumsaidia kufika kwa wakati shuleni akiwa hajachoka ili apate nafasi ya kujifunza na kuelewa.

Aidha Dolice ametoa rai kwa walimu kuwa wazalendo wa kweli kwa kuacha mara moja tabia mbaya ya kujiingiza kwenye mahusiano na wanafunzi ambapo kitendo hicho kinaharibu akili ya mtoto nakusababisha kupoteza kujiamini kwao hatimaye kuleta matokeo mabaya.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages