Breaking

Friday, 31 January 2025

SERIKALI YAOMBWA KUORODHESHA MAPOROMOKO YA MAJI YA KALAMBO KWENYE ORODHA YA URITHI WA DUNIA WA UNESCO

  Na Mwandishi Wetu, Kalambo, Rukwa

Maporomoko ya Maji ya Kalambo (Kalambo WaterFalls), moja ya maajabu ya asili yaliyozungukwa na uoto wa kijani kibichi na hewa safi!

Kutokana na umuhimu huu Serikali imeombwa kuorodhesha maporomoko hayo ya Maji ya Kalambo mkoani Rukwa kwenye orodha ya Urithi wa Dunia wa UNESCO ili kuchagiza utalii na kutengeneza fursa za ajira kwa vijana na wanawake mkoani humo.

Wito huo umetolewa wilayani Kalambo Januari 30,2025 na Mkurugenzi wa TAMCODE Bi. Rose Ngunangwa wakati wa ziara ya shirika hilo pamoja na waandishi wa habari iliyofanywa kwa ufadhili wa UNESCO- Alwalweed Philanthropies.

Bi. Ngunangwa amesisitiza kuwa, uorodheshaji huu utachochea ukuaji wa sekta ya utalii, kuongeza fursa za ajira, na kuboresha maisha ya wanawake na vijana mkoani Rukwa.

Maporomoko ya Kalambo, yenye urefu wa mita 235 (futi 772), ni ya pili kwa urefu barani Afrika, na ni moja ya sehemu chache duniani zinazozungukwa na misitu ya asili isiyoingiliwa na shughuli za kibinadamu. 

Pamoja na uzuri wake wa kipekee, eneo hili linatoa nafasi kubwa ya kutangaza utalii wa kipekee na kuchangia katika uchumi wa taifa.

Mali Asilia na Fursa za Ajira

Bi. Ngunangwa ameonyesha matumaini kuwa ikiwa maporomoko ya Kalambo yatapewa hadhi ya kimataifa, yatavutia wawekezaji kutoka sekta ya umma na binafsi, na hivyo kuongeza idadi ya hoteli, migahawa, na huduma nyingine muhimu za utalii. 

“Hii ni fursa kubwa kwa vijana na wanawake wa mkoa wa Rukwa kupata ajira na kuboresha hali zao za maisha. Kutangaza urithi huu duniani kote kutawawezesha kupata nafasi nyingi za kazi katika sekta ya utalii. Hivyo ni vyema Wizara ya Utalii na Maliasili ikachagiza wawekezaji kutoka katika sekta ya umma na binafsi,” amesema Bi. Ngunangwa.

Miundombinu Inaboreshwa kwa Urahisi wa Kufika

Hata hivyo, changamoto ya awali ilikuwa ni miundombinu, ambapo kumekuwa na ugumu wa kufika kwenye maporomoko haya kwa asilimia mia moja. Lakini kwa sasa, serikali imejenga ngazi 1,270 zinazoshuka hadi kwenye maporomoko, na kufanya eneo hili kufikika kwa urahisi zaidi kwa watalii na wageni.

 Afisa Michezo na Utamaduni wa Mkoa wa Rukwa, Adam Evarist, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi hizi za kuboresha miundombinu, huku akisema ipo haja ya kutunza mazingira ya eneo hili ili urithi huu uendelee kuwepo kwa vizazi vijavyo.

Kutunza Misitu na Kuhifadhi Utamaduni

Ziara hii iliyofanyika mkoani Rukwa, imejumuisha waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari vya kijamii na kidigitali, watendaji wa TAMCODE, na maafisa kutoka Manispaa ya Sumbawanga ili kuchagiza umuhimu wa kutunza misitu, utalii na urithishwaji wa utamaduni usioshikika na unaoshikika.

Wamejadili pia umuhimu wa kutunza misitu na kuendeleza urithi wa kiutamaduni unaoshikika na usioshikika. 

“Tutakapolinda mazingira, tutahakikisha kwamba maporomoko haya yanatufaa kwa vizazi vijavyo, na kuwa sehemu ya urithi wa dunia,” amesema Ngunangwa.

Kalambo: Alama ya Utalii wa Kimataifa

Kwa sasa, rasilimali hii ya asili inahitaji kuenziwa zaidi na kuletwa kwenye mwanga wa kimataifa. Kutambuliwa kwake na UNESCO kutazidi kuongeza hadhi yake, na pengine kuwa kivutio cha utalii kinachohusisha wageni kutoka kila kona ya dunia.

Katika mwanga wa juhudi hizi, mkoa wa Rukwa unaonekana kuwa na nafasi ya kipekee ya kuandika historia mpya ya maendeleo kupitia utalii endelevu, ambao utaongeza fursa za ajira, kuboresha uchumi wa mkoa, na kuchangia katika ustawi wa taifa kwa ujumla.



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages