-Kuuzwa kwa shilingi 19,500 tu
-Kaya 16,275 kunufaika
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeingia mkataba na mtoa huduma Kampuni ya Taifa Gas Limited kwa ajili ya kutekeleza mradi wa shilingi milioni 317.3 wa kusambaza majiko ya gesi 16,275 (LPG) ya kilo sita kwa bei ya ruzuku ya 50% sawa na shilingi 19,500 kwa jiko katika maeneo ya vijijini Mkoani Lindi.
Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi REA, Mhandisi Emanuel Yesaya amebainisha hayo Januari 3, 2025 Mkoani Lindi wakati wa kumtambulisha mtoa huduma huyo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
"Ili kufikia azma ya Serikali kupitia Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 ya kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati kupikia; REA tumekuja na programu hii ya kusambaza majiko ya gesi ya kilo sita kwa bei ya ruzuku," alisema Mhandisi Yesaya.
Alisema kuwa lengo la mradi huo ni kukuza, kuchochea, kuwezesha na kuboresha upatikanaji wa huduma za Nishati Safi ya kupikia ili kupunguza ukataji miti.
"Mradi huu unakwenda kusaidia kuondokana na athari za kiafya, pia utasaidia kuepuka vitendo vya kikatili, kulinda vyanzo vya maji na kutunza Mazingira na pia kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa inayosababisha mabadiliko ya tabia ya nchi," alifafanua Mhandisi Yesaya.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Zuwena Jiri amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi huo wa majiko ya ruzuku ambao alisema utaongeza matumizi ya nishati safi kupikia hususan kwa wananchi wa maeneo ya vijijini.
"Tumefurahi kupata mradi huu; tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na tutaendelea kuhamasisha wananchi kuachana na matumizi ya nishati zisizo kuwa safi na salama ili kulinda afya na mazingira," alisema.
Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kujaza mitungi pale inapoishiwa gesi ili kuendelea kutumia.
Alimuelekeza Mtoa huduma (Taifa Gas) kuhakikisha anakuwa na mawakala kwenye kila kata na vijiji ili kumrahishia mwananchi kubadilisha mtungi pale gesi inapomalizika.
"Ili kuwa na uendelevu wa matumizi ya gesi kupikia, natoa wito kwa Taifa Gas kuwa na mawakala ili kumrahishia mwananchi; tusikubali kumpoteza mtu kurudi kwenye kuni na mkaa kwa sababu ya kukosa mahala pa kubadili mtungi," alielekeza.
Kwa upande wake, Meneja mauzo wa Taifa Gas Kanda ya Kusini, Hawa Omari alithibitisha kuwa wanejipanga vyema kufika kwenye maeneo yote Mkoani hapo sambamba na kutoa elimu kwa wananchi watakaonunua majiko hayo kabla ya kutumia.