Breaking

Tuesday, 28 January 2025

GCLA YAPONGEZWA KWA KUSAIDIA UPATIKANAJI WA HAKI

Na Oscar Nkembo

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kazi kubwa inayofanya katika upatikanaji wa haki Jinai nchini Tanzania huku akifurahishwa na utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka kwa ujumla.

Prof. Gabriel ametoa pongezi hizo katika maonesho ya wiki ya Sheria yanayofanyika katika viwanja vya Nyerere Square, jiji Dodoma wakati alipotembelea banda la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ambapo amesema GCLA inafanyakazi kubwa sana ambayo Serikali inatambua na kuiomba Mamlaka iwekeze nguvu kubwa kujitangaza katika vyombo vya habari

“GCLA inafanyakazi kubwa sana katika upatikanaji wa haki jinai nchini lakini vilevile kwenye utekelezaji wa majukumu yake kwa ujumla, wito wangu naomba wajikite kujitangaza kwenye vyombo vya habari ili wananchi wajue kazi kubwa wanayoifanya” alisema Prof. Gabriel

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Sayansi Jinai, David Elias, amesema katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2025 inayomalizika mwezi Desemba, Serikali imewekeza rasilimali za kutosha hali iliyosaidia kufanyika maboresho makubwa katika utendaji kazi wa Mamlaka

“Serikali imeboresha kwa kiwango kikubwa sana utendaji wa Mamlaka kwa kununua Mitambo ya Kisasa ambapo tofauti na awali kwa sasa matokeo ya uchunguzi yanatoka kwa wakati bila kuchelewa, kuelekea Dira ya Taifa 2025 maboresho makubwa zaidi yanafanyika katika mifumo ikiwemo kuunganishwa kwa mifumo yaTEHAMA kwa wadau wa haki jinai ikiwemo Jeshi la Polisi ili kuwa na uwezo wa kufuatilia mwenendo wa sampuli kutoka inapofika mpaka matokeo yanapotoka” alisema Elias.

Katibu Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Olle Gabriel (kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi wa Huduma za Sayansi Jinai wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, David Elias (kulia) wakati alipotembelea banda la Mamlaka katika maonesho ya wiki ya Sheria yanayofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma Januari 27, 2025.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa pili kushoto) akitoa pongezi kwa GCLA kwa utoaji huduma bora za uchunguzi wa kimaabara wa sampuli za jinai wakati alipotembelea banda la Mamlaka katika maonesho ya wiki ya Sheria yanayofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma, Januari 27, 2025. Kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Sayansi Jinai kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, David Elias.

Mtumishi wa Mamlaka, Sadock Mboya (kulia) akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika maonesho ya wiki ya Sheria yanayofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma Januari 27, 2025.
Mtumishi wa Mamlaka, Aston Nathan (kushoto) akijibu maswali ya mwananchi aliyetembelea banda la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika maonesho ya wiki ya Sheria yanayofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma Januari 27, 2025.Mlimbwende wa Dodoma “Miss Dodoma”, Tibah Adam (katikati) akipokea Elimu katika banda la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika maonesho ya wiki ya Sheria yanayofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma Januari 27, 2025.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages