Thursday, 5 December 2024

WAZIRI MKUU AKOSHWA NA TAFITI YA MHITIMU WA OUT

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa, ameonesha kuvutiwa na utafiti uliofanywa na mhitimu wa Shahada ya Uzamivu (PhD) wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Marehemu Billy Mwakatage kwa kuiagiza Idara ya Menejimenti ya Maafa na Jeshi la Zimamoto kutumia mapendekezo yaliyomo kwenye utafiti huo katika kukabiliana na majanga nchini.

Waziri Mkuu, ametoa wito huo Disemba 05, 2024 katika mahafali ya 43 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambapo alimwakilisha Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango yaliyofanyika katika viwanja vya Kawawa katika Manispaa ya Kigoma-Ujiji.

Shahada hiyo imepokelewa na Mjane wa Marehemu Bi. Ningile Kapange kutokana na Bw. Mwakatage kufariki kabla ya kutunukiwa shahada yake, Waziri mkuu amesema tafiti yake ina mahusiano makubwa na shughuli inayofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa katika kudhibiti maafa na majanga mbalimbali.

“Kwa kuwa ameshahitimu na leo anapata shahada na amefanya utafiti wa kina kwenye eneo la maafa na hasa majanga ya moto ambayo wakati wote serikali tumekuwa tukipambana nayo, msomi wetu Marehemu Billy Mwakatage pamoja na utafiti ametoa mapendekezo mbalimbali, utafiti huu uchukuliwe na ufanyiwe kazi katika kukabiliana na majanga hapa nchini,” amesisitiza Mh. Majaliwa.

Aidha, Mh. Majaliwa amekipongeza chuo hiki kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutekeleza miradi mbalimbali ya Elimu ya Juu ambayo inalenga kuleta mageuzi ya kiuchumi ambapo chuo kimepewa dola za Marekani milioni tisa sawa na shilingi bilioni 23 za Kitanzania kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi ambao unakwenda kuzalisha wataalamu wenye uwezo wa kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo, ufugaji na utalii ili kuongeza kasi ya Taifa letu kujikomboa kiuchumi.

Akiongea katika mahafali hiyo, Mwenyekiti wa Baraza la chuo, Prof. Joseph Kuzilwa, amesema chuo kimeendesha uchakataji wa mitaala na kuanzisha mitaala mipya ili kuendana na mabadiliko ya Sera ya Elimu ya 2014 iliyohuishwa 2023 ikiwa ni maono ya serikali ya awamu ya sita katika kuleta mageuzi ya elimu ili iendane na mahitaji halisi ya maendeleo ya sasa na baadae.

“Tunaishukuru sana serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo inahakikisha shughuli za chuo hiki hazikwami ili mazingira ya ufundishaji na kujifunza yaweze kuimarika, kuthibitisha hayo serikali imeipatia chuo majengo matano katika mikoa ya Lindi, Simiyu, Geita, Kigoma na Manyara.” Amesema Prof. Kuzilwa.

Akiongea kwa niaba ya Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Katibu Mkuu wa wizara hiyo Prof. Carolyne Nombo, amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema chuo hiki kimekuwa na mchango mkubwa kwa nchi kwa kipindi chote cha miaka 30 ya utoaji wake wa huduma kwa kushiriki kutengeneza rasilimali watu ya Watanzania ambao wanaweza kutatua changamoto za nchi yetu.

“Chuo hiki kinatimiza miaka thelathini mwaka huu, wizara imekuwa ikifanya kazi kwa ukaribu na chuo hiki katika miradi mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) wenye thamani ya shilingi bilioni 972 ambapo chuo hiki kimetengewa shilingi bilioni 23 kwa ajili ya ujenzi wa maabara, kufanya mapitio ya mitaala, kusomesha wahadhiri na kuendesha program maalum za kuwapatia sifa wasichana wanaosoma masomo ya sayansi na wanaotoka katika mazingira magumu kujiunga na elimu ya juu, lengo ni kupata rasilimali watu ya watanzania mabao ni makini na mahiri watakaoweza kutatua changomoto zinazowakabili wananchi na nchi yetu,” amesema Prof. Nombo.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda, amesema utaratibu wa kufanya mahafali katika mikoa mbalimbali una lengo la kuwataarifu wananchi kuwa chuo hiki kipo katika kila mkoa na ubora wa elimu yake umekubalika ndani na nje ya nchi. Aidha ameishukuru serikali kwa kuendelea kukiunga mkono chuo hiki kwa kukipatia fedha za maendeleo na miradi mbalimbali inayoendelea kukiimarisha chuo hiki katika maeneo mbalimbali ikiwemo miundombinu na teknolojia ambapo ubora huu unazidi kupasua anga kiasi cha kualikwa katika nchi mbalimbali kuendesha mafunzo kwa wananchi na taasisi zinazotaka kupata uzoefu kutoka katika chuo hiki.

Mahafali ya 43 ambayo ndiyo mahafali ya mwisho kwa Makamu Mkuu wa chuo hiki Prof. Elifas Bisanda anayekwenda kustaafu hivi karibuni, wahitimu wapatao 4307 wanahitimu katika kozi mbalimbali ambapo kati yao wahitimu 2070 ni wanawake sawa na 48.1% ukilinganisha na mahafali ya 42 yaliyofanyika Songea, Ruvuma ambapo wanawake walikuwa 44%.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages