Breaking

Saturday, 21 December 2024

TBS YAWATAKA WAINGIZAJI WA BIDHAA ZA CHAKULA NA VIPODOZI KUSAJILI BIDHAA ZAO

WAFANYABIASHARA wanaoingiza bidhaa za chakula na vipodozi kutoka nje ya nchi wametakiwa kusajili bidhaa hizo Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kwa kuwa kufanya hivyo ni kutekeleza matakwa ya sheria.

Wito huo umetolewa na Meneja wa Usajili wa Bidhaa na Majengo wa TBS kutoka Idara ya Udhibiti Ubora TBS, Habakuki Kalebo, wakati akizugumza na waandishi wa habari, leo Desemba 19,2024 jijini Dar es Salaam.

Amesema usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi unafanyika kupitia mfumo wa Online wa TBS ambao unaitwa OAS, ambapo ili mtu aweze kusajili bidhaa zake anatakiwa kujisajili kupitia mfumo huo.

Amesema usajili wa bidhaa na majengo ya biashara ni takwa la kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Viwango 2 ya Mwaka 2009 ambayo imefanyiwa mabadiliko katika Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019.

Kalebo amesema kwa mujibu wa sheria hiyo mfanyabiashara yeyote yule anatakiwa kusajili bidhaa zake chakula, lakini pia kusajili na majengo.

"Sheria hii inasema mtu yeyote yule haruhusiwi kuzalisha, kuingiza bidhaa ya chakula au vipodozi ndani ya nchi wala kusambaza, wala kuuzwa kabla bidhaa hiyo haijasajiliwa na TBS," amesema Kalebo.

Aidha, amesema sheria hiyo inaeleza kwamba mtu yeyote yule haruhusiwi kuuza, kusambaza au kuhifadhi chakula au vipodozi katika jengo lolote lile ambalo halijasajiliwa na TBS .

Amefafanua kuwa hiyo inafanyika ili kulinda ubora wa bidhaa, usalama na kulinda umma ili uweze kutumia bidhaa ambazo ni salama kwa lengo la kulinda afya za watumiaji.

"Umuhimu wa kusajili bidhaa ni kuhakikisha ubora umezingatiwa na umehakikiwa vizuri na kuhakikisha usalama wa bidhaa hizo umezingatiwa vizuri.

Ikumbukwe kuwa hizo bidhaa watu wanakula zinaingia ndani ya mwili, kwa hiyo zisipokuwa zimethibitishwa ubora wake, kuthibitishwa usalama wake zitakuwa na athari kubwa kwenye afya za watu na zinaweza kupelekea kifo pamoja na magonjwa mengine.

Kwa hiyo lengo la TBS ni kuhakikisha bidhaa zote zinazoingia lazima ziwe zinakidhi hayo matakwa, iwapo mwananchi atanunua bidhaa ambazo hazijatibitishwa anaweza kukutana na madhara ya kiafya." Amesema

Ametoa wito kwa wananchi wanapokwenda kununua biadhaa kuangalia kama bidhaa hiyo ina nembo ya ubora ya TBS. " Lakini bidhaa ambazo tunazisajili kutoka nje ya nchi kuna zile ambazo zina nembo ya ubora na zile ambazo hazina nembo ya ubora," amesema.

Aidha, amesema usajili wa bidhaa ambazo zinazalishwa ndani ya nchi unafanyika kukupitia utaratibu unaoitwa Product Certification kwa kuwapatia leseni wazalishaji yakutumia nemno ya ubora na hapo moja wanakuwa wamesajili kupitia huo utaratibu.

Kwa upande wa majengo, Kalebo amesema yanasajiliwa ili kuhakikisha bidhaa za vipodozi pamoja na bidhaa za vyakula haziathiriwi na mazingira ambayo vinatunzwa .

"Kwa hiyo tunakagua majengo ili kujiridhisha kuwa yana mazingira ambayo ni wezeshi ambayo hayasababisha kuharibika kwa ubora na usalama wa bidhaa husika," amesema Kalebo,

Ameongeza kwamba bidhaa zozote zile ambazo zinagundulika zimeingia nchini kinyemela na zile ambazo huenda zina madhara kwa watumiaji kama vile vipodozi ambavyo vinakuwa na viambato sumu, TBS huwa inahuwisha taarifa hizo kwenye kanzi data yake kila mwezi na kuorodhesha bidhaa zile ambazo zinaonekana zilikuwa na viambata sumu na hazitakiwi kutumika nchini.

Ameongeza kwamba wananchi wanashauriwa kutembelea tuvuti ya TBS kuweza kujua bidhaa ambazo zimesajiliwa na shirika hilo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages