Breaking

Thursday, 5 December 2024

TBS YAELEZA MAFANIKIO YA UDHIBITI WA BIDHAA HAFIFU KWENYE MKUTANO WA KIKANDA WA MATUMIZI BORA YA NIAHATI ARUSHA





SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS),limeeleza namna lilivyofanikiwa kupunguza uingizwaji na uzalishaji wa bidhaa hafifu zisizo na viwango hapa nchini ,kutokana na uwekezaji mkubwa wa vifaa vya kisasa vya upimaji.

Akiongea na waandishi wa habari katika banda la maonyesho la TBS wakati wa mkutano wa kikanda wa Matumizi bora ya Nishati (REEC 2024) unaofanyika jijini Arusha,Msimamizi wa kamati wa kitaalamu ya uandaaji wa Viwango,Peter Maliwa alisema mafanikio hayo yametokana na elimu wanayoitoa kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa na wanaozalisha hapa nchini.

Maliwa alisema uwekezaji mkubwa wa vifaa vya kisasa vya upimaji uliofanywa na serikali katika shirika hilo ,imesaidia kubaini kwa haraka bidhaa hafifu na kuzikamata kabla hazijaingia kwenye mzunguko wa matumizi ya binadamu.


"TBS tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza uwepo wa bidhaa hafifu hususani vifaa vinavyotumia nishati ya umeme baada ya serikali kutia mkono kwa kuwekeza vifaa vya kisasa vya upimaji" alisema


Alisema pamoja na sheria kuwaruhusu kukamata na kuteketeza bidhaa hafifu zinazoingizwa sokoni ,ama kurejeshwa zilipotoka, wamedai kipaumbele chao ni kutoa elimu kwa wafanyabiashara jambo ambalo limeleta manufaa.

"Katika Maonyesho haya, TBS tumekuja kueleza kazi zetu ikiwa ni pamoja na kuonyesha vitendea kazi vyetu vya kisasa na namna ya uandaaji viwango, upimaji wa bidhaa zinazoingia na kuzalishwa nchini,hivyo uwekezaji huu utamfanya mwananchi atumie bidhaa halisi tofauti na kipindi cha nyuma "amesema


Maliwa aliishukuru serikali kwa namna ilivyowekeza vifaa vya kisasa vya upimaji katika shirika hilo, hali iliyosaidia kupunguza uwepo wa bidhaa hafifu hapa nchini.


Aidha alisema Mkakati wa shirika hilo ni kuendelea kuwekeza katika uboreshaji na ujenzi wa maabara mpya za kisasa pamoja na kuwa na wataalamu wa kutosha.


"Mkakati uliopo kwa sasa ni kuboresha maabara zetu kwa kuweka vifaa vya kisasa vya upimaji, hadi sasa katika makao yetu makuu yaliyopo Ubungo Dar es laam tuna maabara nane kubwa na tunatarajia kujenga maabara zingine katika jengo letu Mkoani Dodoma"Alisema.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages