Wenyeviti wa vijiji vilivyopo jirani na mgodi wa Barrick North Mara wakionyesha mifano ya hundi za malipo ya gawio la mrahaba la shilingi bilioni 2.1 lililotolewa na Mgodi huo, baada ya kukabidhiwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt Dorothy Gwajima (wa pili kulia waliokaa), katikati ni Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Apolinary Lyambiko.
Baadhi ya viongozi wa vijiji wakipokea hundi za gawio kutoka Waziri Doroth wakati wa hafla hiyo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima akiongea na Wananchi katika hafla hiyo.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara,Apolinary Lyambiko akizungumza
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima akigawa majiko ya gesi kwa baadhi ya akina mama yaliyotolewa na Taifa Gesi kwa kushirikiana na Mgodi huo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima akipata maelezo katika Banda la maonesho la Barrick North Mara wakati wa maonesho ya kuhitimisha maadhimisho ya Siku 16 za kupinga vitendo vya Ukatili wa Kijinsia.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Mgodi wa North Mara katika picha ya pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima.
***
Mgodi wa Barrick North Mara uliopo wilayani Tarime mkoani Mara, kwa mara nyingine tena umevipatia vijiji vitano vilivyo jirani gawio la mrabaha la shilingi bilioni 2.1, ikiwa ni malipo ya robo ya tatu ya mwaka 2024.
Kiasi cha fedha zilizolipwa kwenye vijiji hivyo ni Genkuru (746,461,112), Nyangoto (581,176,695), Kerende (454,221,570), Nyamwaga (225,997,310) na Kewanja (98,350,773).
Wanufaika wa malipo hayo ni vijiji ambavyo vilikuwa na haki ya kuchimba dhahabu kwenye shimo la Nyabigena (ambalo ni sehemu ya mgodi wa North Mara) kabla ya Kampuni ya Barrick kukabidhiwa kuendesha mgodi huo kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals kuanzia mwaka 2019.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko, akiongea katika hafla ya kukabidhi fedha hizo amesema malipo hayo ya shilingi bilioni 2.1 yanafanya gawio la mirabaha iliyotolewa kwa vijiji hivyo kutokana na uzalishaji wa Aprili 2023 hadi Septemba 2024 kufikia shilingi bilioni 4.471.
Mifano ya hundi zenye thamani ya shilingi bilioni 2.1 imekabidhiwa kwa viongozi wa vijiji hivyo na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt Dorothy Gwajima wakati wa maadhimisho ya kilele cha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyofanyika kitaifa Nyamongo wilayani Tarime, Mara.
Waziri Gwajima ameipongeza Barrick North Mara akisema utoaji wa gawio la mirabaha hiyo unasaidia kuboresha huduma za jamii na kuchochea maendeleo ya kisekta katika vijiji hivyo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara amewataka viongozi wa vijiji vilivyopata fedha hizo za mrabaha kuhakikidha wanashirikisha wananchi kupitia mikutano halali kuibua na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wakati.
Nao wenyeviti wa vijiji vilivyopata mrabaha walishukuru na kuupongeza mgodi wa North Mara kwa namna unavyoendelea kuimarisha mahusiano na jamii inayouzunguka.
"Mgodi umekuwa na mahusiano mazuri na wananchi, hasa kwa kushirikiana katika nyanja za kimichezo na kimaendeleo, pia umekuwa ukitimiza wajibu wa kisheria kama Serikali inavyoelekeza, tunashukuru sana," amesema Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyangoto, Zakaria Machage.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Genkuru, Juma Elias ameushukuru mgodi huo na kuahidi kwenda kushirikiana na wananchi wake kupanga matumizi mazuri ya fedha walizopata kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
"Fedha tunayo, sasa hakuna sababu ya kuchelewesha miradi," amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amekabidhi majiko 222 ya gesi kwa baadhi ya wanawake kutoka vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa North Mara.
Majiko hayo yametolewa na mgodi huo kwa kushirikiana na Kampuni ya Taifa Gas katika kuunga mkono jitihada za serikali za kumtua mama kuni kichwani na kumuepushia adha ya matumizi ya nishati ya kupikia isiyo salama kupitia kampeni ya Barrick na wadau wake katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia zilizomalizika juzi.