UJENZI wa maabara tatu za Sayansi katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kakonko, Kigoma, umeleta hamasa kubwa ya kitaaluma kutokana na kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia.
Maabara hizo za Fizikia, Kemia, na Biolojia, zilizogharimu shilingi milioni 180, zilijengwa kwa ufadhili wa Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) kwa kushirikiana na Mfuko wa Elimu wa Taifa (TEA). Shule hii yenye wanafunzi 270 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne imepata mwamko mpya wa elimu, jambo lililowaletea furaha walimu na wanafunzi.
Mkuu wa shule hiyo, Antoria Paul Nkabo, alisema kukamilika kwa mradi huu kutaongeza hamasa ya wanafunzi kufanya vizuri zaidi katika masomo ya sayansi kutokana na mazingira bora na rafiki ya kujifunzia kwa vitendo.
“Kwa kupata mradi huu, tunakwenda kuongeza ufaulu. Tunatarajia nusu ya wanafunzi(167) watakaoingia kidato cha nne wapate daraja la kwanza katika mitihani yao ya mwisho,” alisema.
Mwalimu wa Kemia na Biolojia, Nikolous Kayombo, aliongeza kuwa awali walifundisha masomo hayo kwa nadharia pekee, lakini sasa, kupitia maabara hizi, wanafunzi wataweza kujifunza kwa vitendo, hivyo kuongeza uelewa na ufaulu wao.
Wanafunzi Zulfa Twaha (Kidato cha Kwanza), Happines Amosi (Kidato cha Tatu), na Sharifat Hamad walitoa shukrani zao kwa UNICEF na TEA kwa kuwapatia maabara hizi muhimu. Walibainisha kuwa maabara hizi zinawawezesha kufanya majaribio mengi ya masomo ya sayansi, jambo linalochochea mafanikio yao kitaaluma.
Mbali na maabara, TEA pia ilitoa ufadhili wa ujenzi wa bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 120 mwaka 2022/2023, kwa gharama ya zaidi ya TZS milioni 142.9.
Mwanafunzi Sharifat alieleza kuwa bweni hilo limeboresha makazi yao, hivyo kuwawezesha kujikita zaidi katika masomo yao.
hule ya Wasichana Kakonko iliyoanzishwa mwaka 2022 ina jumla ya wanafunzi 274, na mwaka 2025 inatarajia kudahili wanafunzi wengine 100 wa kidato cha kwanza, jambo linaloashiria maendeleo endelevu shuleni hapo