WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, amesema Serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuboresha miundombinu ili kuongeza ajira kwa Watanzania.
Akizungumza, Desemba 16, 2024, katika uzinduzi wa muonekano na chupa mpya ya lita moja ya juisi ya African Fruti inayozalishwa na Kompuni ya Bakhresa Food Products Limited (BFPL), Dkt. Jafo amesema sekta binafsi inategemewa kubeba jukumu la kuongeza ajira.
“Serikali haiwezi kuwaajiri watu wote; sekta binafsi ndio nguzo ya kutengeneza ajira. Uwekezaji kama huu unasaidia vijana na wakulima kuongeza uzalishaji,” alisema Dkt. Jafo, akitoa mfano wa uwekezaji wa zaidi ya Sh 700 bilioni wa Bakhresa.
Aliongeza kuwa miundombinu kama reli ya umeme (SGR) na barabara inaimarishwa ili kuchochea uzalishaji viwandani, na kuhimiza Watanzania kupenda bidhaa za ndani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mahusiano wa Bakhresa Group, Hussein Sufian, alisema bidhaa zinazotumia malighafi za ndani huchangia kukuza uchumi.
Aidha alibainisha kuwa Kiwanda hichi kimeongeza uwezo wa kuchakata matunda kutoka tani 50,000 hadi 100,000 kwa mwaka na bidhaa hizo zinauzwa katika mataifa mbalimbali, ikiwemo Kenya, China, na Mashariki ya Kati, zikichangia fedha za kigeni na ajira kwa vijana.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tetra Pak, Jonathan Kinisu, alisifu ushirikiano wa miaka 17 baina ya kampuni hizo, akisema umeleta teknolojia rafiki kwa mazingira na bidhaa bora zisizo na kemikali.
Naye Mtendaji Mkuu wa BFPL, Salim Aziz, alisema malengo ya kampuni hiyo yanaendana na ajenda ya Serikali ya kukuza uchumi kupitia bidhaa za ndani na uundaji wa ajira.